Polisi wawili wasimamishwa kazi

Polisi wawili wa trafiki nchini Afrika Kusini wamesimamishwa kazi na wanakabiliwa na mashtaka ya kuaibisha kikosi cha polisi baada ya video yao "wakila pesa" kusambaa sana mitandao ya kijamii.

Video hiyo inawaonesha polisi hao wawili wakitumia noti za pesa kuchonokoa meno yao na pia kujipangusa, huku muziki wa sauti ya juu ukisikika kwenye gari lao.

Wawili hao wanaonekana pia wakila chakula chao cha mchana kutoka kwenye mikebe ya Styrofoam kwenye sehemu ya kubebea mizigo nyuma ya gari.

Idara ya polisi wa jiji la Ekurhuleni amesema wafanyakazi hao, ambao wamevalia sare rasmi ya polisi wakati huo, wameiaibisha idara hiyo na kwamba vitendo hivyo si vya kistaarabu.

Msemaji wa idara hiyo Wilfred Kgasago amesema wawili hao wamekabidhiwa barua za kuwasimamisha kazi mapema na kwamba watafika katika kamati ya nidhamu Jumanne.

Waziri wa polisi nchini Afrika Kusini Fikile Mbalula alipakia video hiyo kwenye Twitter mwishoni mwa wiki, na akafurahia hali kwamba wawili hao wataadhibiwa.