HAFIDH SALEH.
Meneja wa Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, Hafidh Saleh, alisema lengo la kwenda mapema ni kutaka kuwapa wachezaji nafasi ya kupumzika na kuwa tayari kupambana kusaka ushindi katika mechi hiyo.
Saleh alisema kuwa wachezaji wote walioko Tabora ni wazima na wanaendelea vizuri na programu ya kiufundi ya timu hiyo iliyoko chini ya Mzambia, George Lwandamina.
"Mechi yetu ya kirafiki dhidi ya Rhino Rangers tunayocheza leo (jana) ni sehemu ya mazoezi, kuna wachezaji kocha anataka kuwaona ili ajue uwezo wao kwa ajili ya kujipanga kuelekea mchezo wetu wa Jumapili," alisema meneja huyo.
STAND WALINDA UWANJA
Ili kudhibiti vitendo vya tuhuma kuelekea mchezo dhidi ya mabingwa watetezi, "makomandoo" wa timu ya Stand United wameanza kuulinda Uwanja wa Kambarage.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Kituo na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mbasha Matutu, alisema maandalizi ya mchezo huo yako katika hatua za mwisho na anawataka mashabiki wa pande zote mbili kuwa watulivu.
Matutu alithibitisha kuwapo kwa "makomandoo" wa Stand United ambao wanafanya ulinzi kwenye uwanja huo wakiamini watafanikiwa kuwazuia wapinzani wao "kuuchezea" uwanja huo.
Katika mechi iliyopita, Yanga ambayo Jumamosi iliyopita ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar, ilipoteza mchezo kwenye uwanja huo wa Kambarage.
