MSHTAKIWA wa pili wa kesi ya mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara tajiri na bilionea wa madini ya Tanzanite, Erasto Msuya, Shaibu Said (Mredii), amedai mahakamani kuwa alipelekwa Kituo cha Polisi kinachoitwa Guantamano, nje kidogo ya Jiji la Arusha na kuteswa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.
Pia alidai kuwa baada ya kuhamishiwa Moshi alifungiwa nusu ya kipande cha tofali kwenye sehemu zake za siri, ili akubali kutia saini maelezo ya kukiri kosa la mauaji.
Shahidi huyo wa kwanza wa upande wa utetezi katika kesi ndani ya kesi, aliieleza mahakama hiyo kuwa wakati analazimishwa na polisi kusaini maelezo hayo akiwa Moshi, alinyweshwa pia maji ambayo yanafanya tumbo kuwaka moto na mwili mzima kuwasha.
Akitoa utetezi wake katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mredi alidai kuwa mateso mengine aliyokutana nayo ni kufungiwa bomba la chuma katikati ya miguu na kuning’inizwa kwenye paa la nyumba akiwa amefungwa pingu mkononi, kuchomwa na singe ya bunduki ya SMG kwenye fundo la mguu karibu na unyayo na kuchokonolewa na singe hiyo ndani yake ili akubali kosa na baadaye kuchomwa na pasi ya umeme miguuni.
Alidai mateso hayo ya polisi yamemfanya awe mlemavu mkono wake wa kushoto ambao kutokana na madhila hayo, hivi sasa anatumia dawa za mifupa na maradhi mengine tangu alipokamatwa mwaka 2013 hadi leo.
Aidha, alidai kutokana na madhila hayo, askari polisi waliokuwa wakimtesa ili akubali kutia saini maelezo ya kukiri kosa la kumuua Msuya, walikuwa wakimkanda kila siku kwa maji ya moto ili apate nafuu na kutia saini kama walivyotaka.
Akiwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo namba 12 ya mwaka 2014, Mredii aliieleza mahakama hiyo kwamba wakati anakamatwa na kuhusishwa na mauaji ya Bilionea Msuya, hakuwapo Mererani, Arusha wala Orkolili kulikofanyika mauaji hayo, kwa vile alikuwa shambani kwake mkoa wa Manyara.
Alidai kwamba hata taarifa za kuuawa kwa kupigwa risasi, Erasto Msuya (Bilionea), alizipata kwa njia ya simu akiwa shambani kwake baada ya kupigiwa simu na shemeji wa marehemu, aliyemtaja kwa jina moja la Shujaa.
Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi 22, Agosti 7, mwaka 2013, majira ya saa 6:30 mchana katika eneo la Mijohoroni, kandokando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Mbali na Mredii, wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Sharif Athuman (31), ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mchimbaji mdogo, mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha na Mussa Mangu (30), mkazi wa Shangarai Kwa Mrefu.
Wengine ni Jalila Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Jabir a.k.a “Msudani” (32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata, Wilaya ya Hai, Karim Kihundwa (33), mkazi wa Lawate, Wilaya ya Siha na Alli Musa maarufu “Majeshi”, mkazi wa Babati, mkoani Manyara.
Kesi hiyo ndani ya kesi iliibuliwa wiki iliyopita na Wakili wa Utetezi, Majura Magafu, baada ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, kudai aliteswa na kulazimishwa kutia saini maelezo bila ridhaa yake.
Madai hayo ya mateso yaliyosababisha afya ya mteja wake (Mredii) kuwa mbaya na kulazimika kupelekwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi) na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufani ya KCMC kwa matibabu zaidi, ndiko kulikoibua mgongano wa kisheria na kuanza kesi ndani ya kesi.
Shahidi huyo wa upande wa utetezi (Mredii), aliongozwa kutoa ushahidi na Wakili wake Majura Magafu kuhusu uelewa wake tangu alipokamatwa hadi kufanyiwa mateso hayo na kisha kulazimishwa kusaini maelezo ya kukubali kushiriki mauaji ya Bilionea Msuya. Mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili Magafu: Walipokuchukua askari kutoka Mererani kuja KIA, ulipofika hapo kulitokea kitu gani?
Shahidi: Walipaki gari chini ya mti wa mjohoro na kuniamuru nilale chini kifudifudi.
Wakili Magafu: Baada ya hapo ikawaje?
Shahidi: Nililala hivyo hadi saa 12 jioni nikasikia wanasema twende hivi na nilihisi wanakwenda barabara ya Arusha.
Wakili Magafu: Ulijuaje uko barabara ya KIA kuelekea Arusha?
Shahidi: Nimeizoea hiyo barabara kwa sababu naipita kila siku.
Wakili Magafu: Mlienda mpaka wapi?
Shahidi: Nilipelekwa mpaka Arusha
Wakili Magafu: Ulipofikishwa Arusha nini kilifanyika?
Shahidi: Nilikaa kwenye gari la Polisi kwa saa mbili hivi hadi waliponishusha kwa amri ya afande Samuel ambaye alitoa ushahidi
hapa mahakamani.
Wakili Magafu: Umesema Arusha ulipelekwa ukumbini, hebu tuambie ni jambo gani lilifanyika?
Shahidi: Nilimkuta RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa) Arusha na baadhi ya askari wengine wenye vyeo vikubwa.
Wakili Magafu: Huyo RPC ulikuwa unamfahamu majina yake kabla?
Shahidi: Hapana, nilikuwa namfahamu kwa sura tu
Wakili Magafu: Wakati unapelekwa pale ukumbini Arusha, kulikuwa na askari wangapi?
Shahidi: Walikuwa kama sita au saba
Wakili Magafu: Tusaidie, wakati huo ulikuwa katika hali gani?
Shahidi: Nilikuwa katika hali nzuri, lakini walikuwa wamenifunga pingu za mikono na miguu.
Wakili Magafu: Ulipofikishwa ukumbini uliambiwa nini na hao uliowakuta?
Shahidi: RPC Arusha aliniambia Shaibu tunachotaka hapa ni ushirikiano wako.
Wakili Magafu: Alikwambia anaomba ushirikiano kuhusiana na jambo gani?
Shahidi: Mauaji ya Erasto Msuya
Wakili Magafu: Huyo Erasto Msuya ulikuwa ukimfahamu?
Shahidi: Ndiyo nilikuwa namfahamu ingawa sikuwa na ukaribu naye.
Wakili Magafu: Ulipowajibu kwamba hutambui chochote kuhusiana na tukio hilo, walikuambiaje?
Shahidi: Niliwaambia kwamba sifahamu jambo hilo na siku ya tukio linapofanyika mimi sikuwapo Mererani, Kia wala Arusha.
Wakili Magafu: Baada ya kuwaambia hivyo walikujibu nini?
Shahidi: Waliniuliza taarifa za kuuawa kwa Erasto nilizipata wapi.
Wakili Magafu: Ukawajibu nini?
Shahidi: Niliwaambia nilizisikia baada ya kupigiwa simu kwamba Erasto ameuawa.
Wakili Magafu: Unaweza kukumbuka ni nani alikwambia kwamba Erasto ameuawa?
Shahidi: Nilipata taarifa baada ya kupigiwa simu na shemeji yake Erasto, anaitwa Shujaa.
Wakili Magafu; Ukiwa kule ukumbini Arusha walikwambia nini hao kina RPC na askari wengine?
Shahidi: RPC Arusha aliniambia tunakuonea huruma kwa sababu tukikukabidhi kwa hawa vijana waliokuja na wewe, sijui kama utarudi salama.
Wakili Magafu: Kutokana na kauli hiyo au ushauri huo wa RPC Arusha uligundua nini?
Shahidi: Kwa sababu hao walioniambia hivyo ni viongozi wakubwa niliingiwa na hofu sana.
Wakili Magafu: Baada ya hapo nini kiliendelea?
Shahidi: RCO Ramadhan Ng’anzi (Mkuu wa Upelelezi Mkoa) alitoa amri kwa afande Samuel na kumwambia ondokeni naye.
Wakili Magafu: Baada ya kutolewa hapo ukumbini mlielekea wapi?
Shahidi: Tulielekea kama tunaenda Babati.
Wakili Magafu: Mlienda hadi wapi?
Shahidi: Tulienda hadi uwanja wa Ndege Kisongo, mkoa wa Arusha na tulienda tukaingia upande wa kushoto.
Wakili Magafu: Safari yenu huko iliishia wapi?
Shahidi: Tulienda hadi kwenye mashamba makubwa ambako kuna kituo cha Polisi kule.
Wakili Magafu: Hicho kituo kinaitwaje?
Shahidi: Wao wenyewe Polisi waliniambia unaijua Guantanamo wewe?
Wakili Magafu: Ehee mlipofika huko Guantanamo nini kiliendelea?
Shahidi: Hapo kituoni tulimkuta dada mmoja askari akiwa kaunta na akaambiwa chomoa hiyo redio ya Sub Uffer na switch yake ilete.
Wakili Magafu: Ni nani aliomba hiyo redio ya Sub Uffer?
Shahidi: Ni askari mmoja toka Arusha aliyekuwa ameongozana na askari wa Moshi anaitwa Faustine Mafwele.
Wakili Magafu: Nini kilifuata?
Shahidi: Waliifungulia kwa sauti kubwa hiyo redio na wakanifungua pingu zote za mikononi na miguuni na kuniambia nivue nguo na kubaki kama nilivyozaliwa.
Wakili Magafu: Baada ya kuvua hizo nguo na kubaki kama ulivyozaliwa, walikufanyaje?
Shahidi: Waliniweka chini ya sakafu wakaniambia wao hawana ombi kama wale maofisa wakubwa zao ila wao wana amri tu.
Wakili Magafu: Wakafanyaje sasa?
Shahidi: Waliniambia sisi hatutaki maelezo wala kinachohusiana na mauaji ya Erasto.
Wakili Magafu: Wakati wakikueleza hayo walikuwa wana nini na nini?
Shahidi: Walikuwa na makaratasi mengi sana
Wakili Magafu: Walikuambia kitu gani kuhusiana na hayo makaratasi?
Shahidi: Waliniambia tunachotaka hapa ni sahihi yako tu.
Wakili Magafu: Baada ya kuwajibu hivyo walifanya kitu gani?
Shahidi: Nilisikia maumivu makali baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani.
Wakili Magafu: Baada ya kukupiga kichwani kuna nini kingine walifanya?
Shahidi: Niliingizwa bomba la chuma katikati ya miguu na yule shahidi aliyetoa ushahidi wake jana (afande Dereck) na mwenzake afande Chilumba akanishika kiuno na kuniweka kwenye meza na kilichoendelea hapo mheshimiwa nilikuwa nakomeshwa na waliniambia hapa salama yako ni sahihi.
Wakili Magafu: Baada ya kuingizwa bomba walifanyaje?
Shahidi: Afande Chilumba alimwambia Dereck jisevie.
Wakili Magafu: Baada ya hapo walifanya kitu gani?
Shahidi: Nilipigwa kwenye nyayo kwa juu (kwenye kifundo) na nilipiga kelele sana.
Wakili Magafu: Sasa hebu tusaidie ile redio ilikuwa na kazi gani?
Shahidi: Yule askari wa Arusha Faustine Mafwele alikuwa anaongeza sauti ili kuzima sauti yangu ibaki ya redio.
Wakili Magafu: Tusaidie ukiwa Moshi, unasema RCO aliondoka kwa hasira baada ya kuambiwa hujasaini, kwani mliondoka kuelekea wapi?
Shahidi: Mashamba ya miwa TPC
Wakili Magafu: Mlipofika mashamba ya miwa kulitokea nini?
Shahidi: Waliniambia sali sala yako ya mwisho
Wakili Magafu: Ulisali?
Shahidi: Nilisali kwa sababu kwenye moyo wangu nilishamwambia Mungu lolote linaweza kutokea na tayari nilikuwa nimeshaweka nadhiri.
Wakili Magafu: Baada ya wewe kumaliza kusali walifanya nini?
Shahidi: Askari mmoja alitoa kitu kama kisu kwenye ncha ya bunduki ya SMG (singe) na kunichoma nayo kwenye unyayo wa mguu.
Wakili Magafu: Walipoingiza hiyo singe kwenye mguu wakafanyaje sasa?
Shahidi: Walikuwa wanaichezesha huko ndani katikati ya mfupa na nyama huku wakiishindilia.
Wakili Magafu: Nini kiliendelea tena?
Shahidi: Walisema wananipeleka kwenye tocha ya mwisho (mateso) na walinipeleka kwenye kituo cha polisi kilichopo karibu na kiwanda cha TPC
Wakili Magafu: Mlipofika kulifanyika kitu gani?
Shahidi: Waliipiga kisu suruali yangu niliyokuwa nimevaa na ikatolewa mwilini.
Wakili Magafu: Wakafanya kitu gani sasa?
Shahidi: Niliona wana kipande cha tofali za block (mchanga) kimefungwa kamba.
Wakili Magafu: Hicho kipande cha tofali kazi yake ilikuwa nini?
Shahidi: Walikichukua wakanifunga kwenye …(sehemu za siri) wakaliacha likiwa linaning’inia huku mimi nikiwa nimefungwa pingu juu ya paa la nyumba.
Wakili Magafu: Hilo zoezi lilichukua muda gani?
Shahidi: Sikuwa najielewa baada ya hapo.
Wakili Magafu: Wakati huo hizo document ulikuwa umeshazisaini?
Shahidi: Kwa sababu niliona nakufa ilibidi nisaini
Baada ya Wakili Magafu kumaliza kumwongoza shahidi huyo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula, alisimama na kumwomba Jaji Salma upande wa utetezi wamwite mahakamani Daktari wa Hospitali ya Mawenzi aje kuhojiwa kuhusiana na matibabu ya Mredii anayedaiwa kuteswa.
“Mheshimiwa Jaji, chini ya kifungu cha 291 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 20 ya Sheria ya Mwaka 2002 iliyofanyiwa marejeo, Daktari Massam E ambaye ana cheo cha AMO (Assistant Medical Officer) aliyejaza fomu namba tatu ya Polisi, aletwe mahakamani kwa ajili ya cross examination (mahojiano),” alidai Chavula.
Kutokana na hoja hiyo ya upande wa mashtaka, Wakili Magafu aliiambia mahakama hiyo kwamba wanatarajia kuleta mashahidi wawili mahakamani akiwamo daktari huyo wa Mawenzi na daktari wa Magereza, hivyo wanaomba wenzao wawe wavumilivu.
Dakika chache baadaye, Wakili Chavula alianza kumhoji shahidi huyo wa kwanza wa upande wa utetezi (Mredii) na mambo yalikuwa hivi:
Wakili Chavula: Nairejesha mahakama nyuma kidogo kwenye kumbukumbu zake, tarehe 10/2/2015 wakati wa PH (Preliminary Hearing), shahidi ukiwa na mawakili wako, kwa nini ulisema ulikamatwa tarehe 15/8/2013, Je, uliidanganya mahakama?
Shahidi: Labda nilikuwa nimesahau.
Wakili Chavula: Umeileza mahakama kwamba tarehe 18/8/2013 ukiwa kizuizini pale Polisi Mererani, baadaye ukapelekwa Polisi Kia, kweli si kweli?
Shahidi: Kweli
Wakili Chavula: Ni sahihi kwamba shahidi wa nne, afande Dereck alikuwa miongoni mwa waliokutesa kutoka Guantanamo hadi mashamba ya TPC?
Shahidi: Ni sahihi.
Wakili Chavula: Kwa nini jana, hamkumuuliza maswali wakati anaitwa kutoa ushahidi wake kwamba alihusikaje kukutesa?
Shahidi: Jaji ndio anajua kwa sababu alikuwa hajaruhusu hilo.
Wakili Chavula: Ni sahihi kwamba wakati Erasto anauawa haukuwa Mererani, Arusha wala Orkalili?
Shahidi: Sahihi.
Jopo la mawakili wa utetezi katika kesi hiyo linaongozwa na wakili Hudson Ndusyepo anayemtetea mshitakiwa wa kwanza, Majura Magafu anayemtetea mshitakiwa wa pili na wa tano, Wakili Emmanuel Safari anayemtetea mshitakiwa wa tatu na John Lundu anayemtetea mshitakiwa wanne, sita na saba.
Upande wa mashtaka katika kesi hiyo ambayo ni gumzo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, unaongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdala Chavula.
Hadi sasa jumla ya mashahidi 10 wa upande wa mashtaka, wameshatoa ushahidi wao mahakamani hapo akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Hai, (OC-CID) Joash Yohana, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai (DMO) Dk. Paul Chaote (39) na Khalid Sankamula (49) ambaye ni Mganga wa Kienyeji na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Limbula, Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora.
Wengine ni Anase Khalid (37), mkulima na mkazi wa Kaliua, Tabora, Mbazi Steven (32), mkazi wa Arusha na Ofisa Upelelezi, Kitengo cha Intelijensia ya Jinai mkoa wa Kilimanjaro, Herman Ngurukisi (40), Inspekta Samueli Maimu (45) ambaye alikuwa kiongozi wa timu ya ukaguzi ya Polisi (CRT) kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa mkoa wa Kilimanjaro na Ofisa Upelelezi (Detective), Sajenti Atway Omari ambaye aliyekuwa katika timu ya CRT. Kesi hiyo itaendelea tena leo.