Diallo ameitaka Serikali kutoingilia masuala ya uchaguzi CCM


      Mwanza/Moro. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo, ambaye mwishoni mwa wiki alipekuliwa na maofisa wa Takukuru, ameitaka Serikali kutoingilia masuala ya uchaguzi wa chama hicho, badala yake iangalie na kuwaongoza wanapokosea.

Diallo alitoa kauli hiyo juzi usiku wakati akiwashukuru wajumbe wa CCM waliomchagua kwa mara nyingine na kusema umefika wakati chama kitafute utaratibu mahsusi kwa viongozi wa kiserikali kuacha kuingilia masuala ya uchaguzi.

“Kuna umuhimu wa kutengeneza kiapo kitakachosaidia Serikali kutoingilia masuala ya uchaguzi bali waangalie na kutuongoza pale tunapoenda kinyume,” alisema.

Jumamosi, gari la Diallo, ambaye amefanikiwa kutetea kiti chake, lilisimamishwa na maofisa wa Takukuru na baadaye kupekuliwa kabla ya kumuachia aendelee na shughuli za kampeni za uchaguzi wa viongozi wa CCM.

Maofisa hao walipekua gari lake wakati waziri huyo wa zamani akiwa wilayani Ukerewe.

“Kitendo cha gari yangu kusimamishwa na maofisa wa polisi na kuanza kupekuliwa hakijanifurahisha kwani hata mimi najua rushwa ni adui wa haki,” alisema Diallo, ambaye ni mfanyabiashara maarufu anayemiliki vyombo vya habari.

Waliodakwa wachunguzwa

Kuhusu watuhumiwa waliokamatwa wakigawa fedha, mkuu wa Takukuru wa mkoa, Ernest Makale alisema bado wanawashikilia kwa mahojiano zaidi.

Kwa mujibu wa Makale watuhumiwa hao walikamatwa juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, ambako chama hicho kilikuwa kinaendesha uchaguzi huo, wakiwa na Sh400,000 pamoja na vielelezo vinavyoonyesha kata zitakazogawiwa fedha hizo.

“Japokuwa wamedhaminiwa na watu wanaoaminika, lakini bado tunafanya nao mahojiano na punde uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani,” alisema Makale. Mbali na watuhumiwa hao, pia alisema wapo wengine ambao idadi yao hakuitaja wanaoendelea kuhojiwa.

“Tunapenda chaguzi ziwe zinafanyika kwa haki na wajumbe wachague viongozi watakaowatumikia kwa moyo,” alisema Makale.

Chadema yaitesa CCM Moro

Mkoani Morogoro, mwenyekiti aliyechaguliwa kuongoza CCM katika mkoa, Innocent Kalogeresi ameahidi kuyarudisha majimbo matatu ya ubunge yaliyochukuliwa na upinzani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kalogeresi alitoa ahadi hiyo jana baada ya kuchaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa mkoa huo.

Alisema majimbo hayo yalichukuliwa kutokana na ubinafsi wa baadhi ya viongozi wa CCM na kutokuwa na umoja.

Majimbo hayo ni Mikumi, Kilombero na Mlimba ambayo yalichukuliwa na wagombea wa Chadema.

Alisema ushindi wa wapinzani ni doa kubwa katika kipindi cha uongozi wake, hivyo katika awamu yake ya pili ya uongozi atahakikisha yanarudi CCM.

“Na hata kata zilizochukuliwa na upinzani nawahakikishia zitarudi zote. Naomba viongozi wenzangu tushirikiane tuache ubinafsi tutangulize masilahi ya chama,” alisema Kalogeresi.

Aliwataka wana-CCM kuweka mbele masilahi ya chama na kuepuka ubinafsi na migogoro isiyokuwa na faida.

Kalogeresi alipata kura 932 na kuwashinda wagombea wenzake ambao ni Said Said aliyepata kura 69 na Elias Mtesa (kura 77).

Pia, Dk Rwekiza alimtangaza Antony Mhando kuwa katibu mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Morogoro.   
Mpya zaidi Nzee zaidi