Serikali imesema ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma utaanza kabla ya Machi na utagharimu dola 1.923 bilioni za Marekani (sawa na Sh4.3 trilioni).
Akizungumza katika kikao cha kuutambulisha mradi huo kwa viongozi wa mkoa huo, meneja mradi wa Kampuni Hodhi ya Raslimali za Reli (Rahco), Maizo Mgedzi alisema unatarajia kuanza wakati wowote kabla ya Machi.
Alisema licha ya treni hiyo kuwa na uwezo wa kwenda kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa, pia itahifadhi mazingira.
Mgedzi alisema itakuwa na uwezo wa kubeba mzigo mkubwa mara tano zaidi ya reli ya sasa.
Meneja wa Kampuni ya Yapi Merkezi iliyopewa zabuni ya mradi huo, Abdullah Kilic alisema jiwe la msingi la mradi huo litawekwa wakati wowote kuanzia sasa.
“Tunachosubiri ni utaratibu wa Ikulu lakini jiwe la msingi tutaliweka wakati wowote kuanzia sasa,” alisema.
Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde alisema Serikali ingependa mradi huo ulete matokeo chanya kwa watu wa Dodoma na si kuwa laana.
“Matokeo haya yasiwe laana kwa maana tusije kuiacha reli hii ipite tu hapana. Tunataka kwa watu wa Dodoma, reli hii iwe kichocheo cha kwanza cha uchumi ikiwezekana kubadilisha mji,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alisema viongozi watawapa ushirikiano wa kutosha katika kipindi cha miaka mitatu cha ujenzi wa reli hiyo na kurekebishana katika baadhi ya mambo.
“Wamesema asilimia 80 (watu 3,000) watachukua watu wa Dodoma kwa hiyo ni jambo kubwa sana. Hii ni fursa kubwa hasa kipindi hiki cha ujenzi,” alisema.
