Dodoma. Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (Talgwu) kimesema kitendo cha Serikali kuwaondoa kazini watumishi 2,490 kwa sababu ya kutokuwa na cheti cha ufaulu cha kidato cha nne ni uonevu.
Akizungumza leo Januari 29, mwaka 2018 katika mkutano wa baraza kuu la chama hicho, ofisa uhusiano wa Talgwu, Shani Kigwasali amesema kwa mujibu wa waraka uliotolewa na Serikali waliopaswa kuwa na vyeti hivyo ni wale walioajiriwa mwaka 2004 na kuendelea.
"Lakini kuna watumishi 2490 waliondolewa kazini kwasababu hiyo huu ni uonevu dhidi ya wanachama wetu," amesema na kubainisha kuwa walioajiriwa kabla ya mwaka 2004 jambo hilo haliwahusu kwa sababu masharti yao ya ajira yalikuwa tofauti.
Amesema chama hicho kimewasiliana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Utumishi bila mafanikio lakini wakati wakiendelea na mazungumzo hayo tayari nafasi za kazi zimetangazwa kwa ajili ya kujaza nafasi zilizoachwa wazi na watumishi hao.
Amesema hata kama Serikali imeamua kuwaondoa kazini lakini utaratibu haukufuatwa kwa kuwalipa stahiki zao.
Mwenyekiti wa chama hicho, Seleman Kikingo amesema maeneo yaliyoguswa yameshaanza kufanyiwa kazi.
"Ni wajibu wetu kuwakumbusha kila mara kuhusiana na changamoto hizi. Wafanyakazi wa Serikali za mitaa tunafanya kazi katika mazingira magumu sana ambayo watumishi wengine wa Serikali hawawezi kufanya kazi," amesema.
Ameitaka Serikali kuangalia upya suala la uundwaji wa halmashauri mpya nchini kwa kufanya tathimini kwanza kabla ya kuzianzisha.
"Wakati mwingine halmashauri zinaanzishwa kwa msukumo wa kisiasa.Tunaomba mliangalie upya kwa kufanya tathimini,"amesema.
Ametoa mfano wa Halmashauri moja mkoani Morogoro ambapo watumishi walienda kurundikwa katika jengo moja.
Akimwakilisha Waziri Mkuu katika ufunguzi wa mkutano huo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Antony Mavunde amesema hoja zote wamezipokea.
Amesema Serikali imeendelea kufanyia kazi changamoto hizo na zile zinazohitaji majadiliano wamekuwa wakifanya hivyo kupitia vikao.
