Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), limeomba vyanzo vya Mto Tarangire kulindwa na kuhifadhiwa kwa kuwa maji yanaendelea kupungua hivyo kutishia maisha ya wanyamapori.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi ametoa wito huo wakati Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, ilipotembelea hifadhi hiyo jana Jumamosi Januari 27,2018.
Amesema maji yanapungua kutokana na kuongezeka shughuli za kibinadamu kando mwa mto na kwenye vyanzo vya maji wilayani Kondoa mkoani Dodoma.
"Tunaomba Bunge na Serikali kuingilia kati kusaidia kulindwa mto huu na vyanzo vyake vya maji kwa kuwa yakipungua ni wazi maisha ya wanyamapori Tarangire yatakuwa hatarini," amesema.
Mkuu wa hifadhi hiyo, Herman Batiho amesema ingawa mvua imeanza kunyesha, bado kiasi cha maji kinachofika katika mto huo ni kidogo.
Amesema kama maji yakipungua wanyama watalazimika kutoka nje ya hifadhi kutafuta maji na malisho hivyo kusababisha adha kwa wananchi na hasa wakulima.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Kemilembe Luota amesema ingawa kuna athari za mabadiliko ya tabia nchi lakini ni lazima kutazamwa umuhimu wa hifadhi.
Amesema ni muhimu Serikali kutazama umuhimu wa hifadhi kwa manufaa ya Taifa, hivyo kuhakikisha wanaofanya shughuli pembezoni mwa mto na kwenye vyanzo vya maji wanaondolewa.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema suala la ulinzi wa vyanzo na maji ni mtambuka na linahusu zaidi ya wizara moja, hivyo ni muhimu Serikali kuwa na msimamo wa pamoja.
