Dk Kalemani afungukia madeni ya taasisi ya Umma

Utoaji huduma usioridhisha wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ni matokeo upungufu wa fedha unaochangiwa na taasisi na mashirika ya umma kulimbikiza mabilioni ya fedha ya madeni ya ankara za umeme zinazodaiwa na shirika hilo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua utoaji wa huduma ya umeme katika kijiji cha Negezi wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga jana Februari 16, 2018, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema Tanesco inadai zaidi ya Sh297 bilioni kutoka mashirika na taasisi za umma.

“Madeni haya yanakwamisha ufanisi wa Tanesco katika usambazaji wa umeme na huduma kwa wateja,” amesema Dk Kalemani.

Akihutubua mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mwamashele wilayani humo, Dk Kalemani amezitaka taasisi na mashirika ya umma yanayodaiwa malimbikizo ya ankara za umeme kulipa ili kuimarisha utendaji wa Tanesco.

Ametoa mfano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama na Shinyanga (Kashwasa) iliyokuwa ikidaiwa zaidi ya Sh2.2 bilioni hadi Tanesco kulazimika kuikatia umeme.

“Tayari Kashwasa wamepunguza deni kwa kulipa Sh800 milioni na mazungumzo yanaendelea kati yao na Tanesco kuhusu muda wa kukamilisha malipo hayo,” alisema Dk Kalemani.

Kaimu Mkurugenzi wa Kashwasa, Lawrence Wasala alisema baada ya kupunguza deni, uongozi wa Tenesco umetoa muda hadi mwishoni mwa mwezi huu kiasi cha Sh1.4 bilioni iliyosalia kulipwa la sivyo huduma itakatwa.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Tellack amemuomba Dk Kalemani kuingilia kati kwa kuiagiza Tanesco kuiongezea Kashwasa muda wa kumalizia deni lililosalia kwani muda uliotolewa wa hadi mwisho wa mwezi ni mfupi.

“Pia wakati wakiendelea kulipa, huduma ya umeme irejeshwe kwenye mashine ya kusukuma maji ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji,” ameomba Tellack.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items