Kamishna Madini afikishwa mahakamani


KAIMU kamishna wa Madini na Katibu wa Bodi ya Ushauri wa Wizara ya Nishati na Madini, Ally Samaje amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka mawili ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka kutoa kibali cha leseni bila baraka za bodi hiyo.

Kadhalika ilidaiwa kuwa mshtakiwa alitoa maelekezo kwa Kamishna Msaidizi wa Leseni na Haki za Madini, John Nayopa kuandaa leseni ya kuchimba madini kwa eneo lenye kilomita za mraba 7.6 kinyume cha sheria za wizara hiyo.

Samaje alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa na alikana mashtaka hayo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai alidai kuwa kati ya Aprili 9 na Juni 21, 2013 Makao Makuu ya Wizara hiyo, Ilala jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa mtumishi wa umma alitumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kuitisha wa bodi na kupata ushauri wake.

Ilidaiwa kuwa hakuitisha mkutano huo kuzingatia maombi ya leseni kwa ajili ya madini aina ya gemstone na mengine unganishi ikiwamo graphite na marble katika eneo la Mererani, Simanjiro mkoani Manyara, yaliyowasilishwa na Kampuni ya Madini ya M/S Tanzaniteone na M/S State Mining Corporation kinyume na sheria ya madini.

Ilidaiwa kuwa  mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa lengo la kuzipatia kampuni hizo faida ya eneo la madini kilomita za mraba 7.6.

Swai alidai katika shtaka la pili, mshtakiwa huyo alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa maelekezo kwa msaidizi wake  Nayopa,  kuandaa leseni ya kuchimba madini hayo bila kuzingatia mfumo wa uendeshaji wa taarifa za madini wa wizara hiyo.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na uliomba tarehe ya kusikiliza maelezo ya awali na kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ametoa kibali cha kuendelea usikilizwaji wake katika mahakama hiyo.

Hakimu alisema kwa kuwa alisema mshtakiwa atakua nje kwa kujidhamini hati ya dhamana ya Sh. milioni 50, wadhamini wawili wanaotoka taasisi inayotambulika, asisafiri kwenda nje ya nchi bila kibali cha mahakama hiyo.

Mshtakiwa alitimiza masharti hayo na yuko nje kwa dhamana hadi Februari 28,mwaka huu mshtakiwa atakaposomewa maelezo ya awali.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items