Mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi ya Tido siku mbili mfululizo


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajiwa kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando kwa siku mbili mfululizo, kuanzia Aprili 24 na 25 mwaka huu.

Mhando anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh. milioni 887.1.

Akiieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Leo, Mwendesha Mashtaka wa taasisi kupambana na kuzuia rushwa (Takukuru) Leonard Swai,  amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa kwa ushahidi wa upande wa mashtaka.

 Ameeleza kuwa kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Victoria Nongwa lakini kwa sasa imepangwa kusikilizwa mbele yake na wataanza na mashahidi wawili kusikilizwa mfululizo yaani Aprili 24, 25 mwaka huu. Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Shaidi amepanga kuisikiliza kesi hiyo Aprili 24 na 25, mwaka huu.

 Miongoni mwa tuhuma zinazomkabili Tido ni kuwa Juni 16, 2008 akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha shughuli za utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.