Ajali za barabarani zilivyowaliza wanahabari nchini


Aliyekuwa Ofisa Habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Hamza Temba amezikwa jana nyumbani kwao Isawerwa kata ya Masama wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro. Hamza anakuwa Ofisa Habari wa pili serikalini kupoteza maisha kwa ajali ya gari ndani ya siku nane.

Marehemu Temba alifariki dunia Jumamosi Agosti 4 kwa ajali ya gari alipokuwa safarini na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla.  Ajali hiyo ilitokea eneo la Magugu mkoani Manyara, huku kiongozi huyo akipata majeraha sehemu mbalimbali za mwili.

Ajali hiyo imekuja ikiwa ni siku nane tangu gari la Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji lilipopata ajali Katoro mkoani Geita na kusababisha kifo cha Ofisa Habari wa Wizara hiyo, Shadrack Sagati, Julai 28.

Ajali hiyo, licha ya kuchukua maisha ya Sagati aliyezikwa Jumamosi Agosti 4, wilayani Bunda, watu wanne walijeruhiwa akiwamo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ludovick Nduhiye; dereva Lucas Wambura; Mchumi wa Wizara, Nickson Matembo na Yusuph Mbwalwa.

Baada ya ajali hiyo, Dkt. Kigwangalla alitibiwa kwa muda katika kituo cha Afya Magugu kisha akasafirishwa kwa helikopta hadi Hospitali ya Selian mkoani Arusha kwa matibabu zaidi na badaye kusafirishwa kuletwa Dar es salaam.

Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Babati, Dkt. Madama Hossea alitaja majina ya majeruhi wa ajali hiyo mbali na waziri kuwa ni mwandishi wa habari Michael Mlingwa (30) na Msaidizi wa Waziri, Ramadhan Magumba (30), huku dereva wa gari hilo Juma Saleh (59) na Katibu wa Waziri, Ephraim Mwangombe (47) hawakupata jeraha lolote na kwamba, walitoka salama kwenye ajali hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Augustine Senga amesema chanzo cha ajali hiyo iliyohusisha watu sita waliokuwa wakisafiri kutoka Arusha kwenda Dodoma ni twiga aliyekatiza barabara ghafla na dereva wa gari katika jitihada za kumkwepa liliyumba kushoto na kulia kisha likapinduka.

Wakati ajali hizo zikiibua mijadala mbalimbali mitandaoni, Waziri  wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola juzi wakati akizindua Baraza la Taifa la Usalama Barabarani,amesema magari ya serikali ndiyo yanayoongoza kwa kuvunja sheria za barabarani na kuwataka viongozi wa umma waonyeshe mfano kufuata sheria.

“Kwa mujibu wa taarifa za Polisi, magari ya serikali na hasa ya viongozi ndiyo yanayoongoza kwa uvunjifu wa sheria, nimeshaagiza askari wa usalama barabarani kukamata tu, wala usiangalie cheo”, amesema Lugola.
Mpya zaidi Nzee zaidi