WAZIRI WA MALIASIALI NA UTALII, DK. HAMISI KIGWANGALLA (KATIKATI), AKIFANYA MAZOEZI YA KUTEMBEA KATIKA VIUNGA VYA UPANGA MASHARIKI, JIJINI DAR ES SALAAM JUZI USIKU AMBAPO ALITEMBEA UMBALI WA KILOMETA NNE. WENGINE NI WASAIDIZI WAKE, KATIBU WA WAZIRI, EPHRAIM MWANGOMO (KULIA) NA RAMADHAN MAGUMBA
Dk. Kigwangalla alifanya mazoezi hayo juzi jioni kwa kutembea umbali huo kisha kupanda jengo la MOI kwa kutumia ngazi kutoka chini mpaka ghorofa ya Sita.
"Kwa sasa naendelea vizuri tofauti na awali nilipokuwa natembea umbali mdogo kutoka Wodi ya Mwaisela nilipokuwa nimelazwa na kutembea mpaka geti la kuingilia hospitali hii ya Muhimbili.
“Kwa sasa natembea umbali mrefu Zaidi. Nilianza na kilomita moja, nikaongeza kilometa moja na nusu na baadae mbili, lakini nikaona leo (juzi) niongeze zaidi na kumaliza kilomita hizi nne,’ alisema.
Aliongeza kuwa: “Mazoezi haya ya kutembea yananisaidia kuimarisha zaidi mapafu. Lakini kwa sasa bado nashughulikia mkono pekee."
Dk. Kigwangalla huanza kufanya mazoezi hayo kila siku jioni kwa lengo la kujiimarisha kiafya pamoja na tiba kwa hali yake hiyo ambayo kwa sasa anaendelea na matibabu.
Kwa upande wao madaktari bingwa wanaomtibu waziri huyo, walibainisha kuwa licha ya kuendelea vizuri, bado wanafuatilia kwa karibu hali ya afya yake hadi watakapojiridhisha ndipo watamruhusu kurejea nyumbani kuendelea na majukumu yake.
Dk. Kigwangalla alipelekwa MOI Agosti 12, mwaka huu, na kufanyiwa upasuaji wa mkono ambao ulivunjika kutokana na ajali aliyoipata Agosti 4, akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Manyara.
