MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Shaaban Iddi Chilunda leo amepata mapokezi mazuri katika klabu yake mpya, CD Tenerife ya Daraja la Kwanza nchini Hispania anayojiunga nayo kwa mkopo wa miaka miwili kutoka Azam FC.
Chilunda amewasili leo na kupokewa na mashabiki kadhaa wa timu hiyo sambamba na kundi kubwa la Waandishi wa Habari waliomfanyia mahojiano makao makuu ya klabu, Santa Cruz de Tenerife, Tenerife, visiwa vya Canary.
Akizungumzia mapokezi hayo, Chilunda aliyepelekwa hadi Uwanja wa Heliodoro RodrÃguez López, unaotumiwa na timu hiyo amesema; “Kwa kweli nimefurahi sana, yamekuwa mapokezi makubwa ambayo sikuyatarajia, namshukuru sana Mungu, hii inanipa ujumbe kwamba nina deni kubwa hapa. Watu wana matarajio makubwa na mimi. Nitajitahidi kwa uwezo wa Mungu,”amesema.
Shaaban Iddi ambaye aliyetimiza miaka 20 Julai 20 mwaka huu tangu azaliwe mwaka 1998, alijiunga na akademi ya Azam FC Jumamosi ya Julak 21, mwaka 2012 kabla ya miaka miwili baadaye kupandishwa kikosi cha kwanza.
Na msimu huu Chilunda ameweka rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kwa kufunga mabao nane, yakiwemo manne ya rekodi katika mchezo mmoja wa Robo Fainali dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda.
