Serikali kuzichukulia hatua kampuni zisizoajiri walemavu


Serikali imesema kuanzia sasa itaanza kuchukua hatua kwa Kampuni mbalimbali ambazo zitakutwa zimevunja Sheria inayowataka kutoa ajira za asilimia 3 ya watu wote walioajiriwa.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera , Bunge , Kazi Vijana na Walemavu Stela Ikupa akiwa na watu wenye ulemavu mkoa wa Tabora pamoja na uongozi wa mkoa baada ya kumaliza kikao nao.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Tabora na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera , Bunge , Kazi Vijana na Walemavu Stela Ikupa baada ya kutembelea Kampuni ya Tanzania Leaf Tobacco Co. Ltd(TLTC) ikiwa mwajiri mmoja wenye ulemavu kati ya watumishi zaidi ya 400.

Alisema Sheria namba 9 ya mwaka 2010 inamtaka mwajiri yoyote anayeajiri watumishi kuanzia 20 kuendelea kuhakikisha asilimia 3 ya watumishi hao ni watu wenye ulemavu.

Naibu Waziri huyo aliwaagiza Afisa Kazi na Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tabora na mikoa mingine kuhakikisha Waajiri wote wanayo Sheria hiyo na wanaitekeleza.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera , Bunge , Kazi Vijana na Walemavu Stela Ikupa, Mkurugenzi mkuu, Mbunge viti maalum mkoa wa Tabora , Mwanne Nchemba pamoja pamoja na wafanyakazi wa kiwanda kiwanda cha maji mazuri 
Alisema baada ya hapo Serikali ikikuta Mwajiri ambaye hakuzingatia matakwa ya Sheria haitasita kumchukulia hatua kwa ubaguzi na hatua dhidi yake zitachukuliwa.

Ikupa aliongeza kuwa hata wakati wa usaili kwa ajili ya nafasi za kazi ni vema wakaweka utaratibu rafiki ambapo unatoa nafasi kwa watu wenye ulemavu ili waweze kupata nafasi za ajira kwa wingi.

Alisema nafasi nyingine ambazo wanaajiriwa watu wasio na ulemavu kazi hizo kama vile za mapokezi zingeweza hata kufanywa na Watu wenye ulemavu kwa ajili ya kujipatia kipato lakini wamekuwa hawapatiwi fursa hiyo.

Wakati huo huo Naibu Waziri huyo alizitaka Kampuni mbalimbali na Ofisi ya Umma kujenga miundombinu ambayo ni rafiki kwa mtu mwenye ulemavu kufanya kazi.

Alisema wakati mwingine miundo mbinu inayojengwa katika majengo mengine inamkatisha tamaa mtu wenye ulemavu wa viungo kufanyakazi na hivyo kushindwa kuendelea na kazi.

Ikupa alisema kwa kuliona hilo Serikali imeanza kufanyia marekebisho majengo yake mbalimbali ili watu wenye ulemavu nao waweze kupata fursa ya kufika kazini au kupeleka shida zao bila vikwanzo.

Naibu Waziri huyo yuko Mkoani Tabora kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa mikataba ya ajira na sheria Na 9 ya mwaka 2010 na kuzungumza na watu wenye ulemavu.
Mpya zaidi Nzee zaidi