Serikali yajipanga kuinusuru Stars


Wakati wadau wa soka nchini wakitofautiana kuhusu uamuzi uliochukuliwa na Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) Mnigeria, Emmanuel Amunike wa kuwatema wachezaji wa Simba katika kikosi chake kinachojiandaa kuivaa Uganda, serikali imeingilia kati suala hilo.

 Mkurugenzi wa Michezo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yusuf Singo alisema kuwa serikali imeanza mazungumzo haraka ili kufikia uamuzi ambao utakuwa na maslahi kwa taifa.

Singo alisema ni mapema kusema nani ndiye mwenye makosa kati ya Amunike, Simba au Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mpaka pale watakaposikia.

"Hatujakaa kimya, tunaendelea kulihangaikia tuone linakaaje," alisema kwa kifupi Singo.

Rais wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage alisema jana kuwa klabu yake haina makosa na uamuzi uliochukuliwa wa kuwaondoa nyota wake katika kikosi cha Stars haukuwa sahihi.

Hata hivyo Rage alisema pia makocha wamekuwa wakali kwa sababu baadhi ya wachezaji wa timu za Taifa za Afrika hawana nidhamu.

"Nadhani mwalimu (Amunike) na TFF wameghafilika, wachezaji wa Simba hawajafanya makosa, walipaswa kupewa onyo," alisema Rage na kueleza kanuni za Fifa zinavyosema.

"Kwa maoni yangu, kocha amewekwa kwenye sehemu si nzuri, namwonea huruma sana, Simba iliwapa wachezaji wake mapumziko ya siku mbili na walipaswa kurejea kambini jana (juzi) Jumatano, wakati mwalimu anawapa ruhusa hakuwa na taarifa kama walitakiwa kuripoti kwenye kambi ya Stars," alisema Crescentius Magori, Makamu wa Rais wa zamani wa TFF.

Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara aliwataka mashabiki wa klabu hiyo kuwa watulivu na jambo hilo linashughulikiwa kwa njia ya kidiplomasia.

Stars inaendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa ugenini wa kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) dhidi ya Uganda utakaofanyika Septemba 8 mwaka huu jijini Kampala.

Mpya zaidi Nzee zaidi