Na Ferdinand Shayo, Kilimanjaro
Serikali imetoa siku 125 kampuni ya ujenzi ya China Geo kukamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya kilomita 32 kutoka Eleraui hadi Sanya juu wilayani Siha mkoani Kilimanjaro baada ya kampuni hiyo kukabiliwa na changamoto nyingi katika kipindi cha utekelezaji wake.
Naibu Waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa amekubali ombi la kuongezewa muda kwa mkandarasi huyo lililotolewa na meneja wa wakala wa barabara (Tanroad) mkoani kilimanjaro mhandisi Nkolate Ntije baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.
Hata hivyo Naibu Waziri ameionya kampuni hiyo kama itashindwa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa muda huo na kuwakwamisha wananchi ambao wamekuwa wakiteseka kutokana na ubovu wa barabara haitapewa tenda ya ujenzi wa barabara nchini .
Meneja wa Wakala wa barabara (Tanroad) mkoani Kilimanjaro Mhandisi Nkolate Ntije amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na mvua nyingi zilizonyesha mwaka huu na ukosefu wa changarawe baada ya wenye machimbo ya changarawe ambao wana hati miliki kuzuia wakidai walipwe kwanza fidia.
Wananchi wa wilaya hiyo Wilson Mushi wameishukuru serikali kwa kuwajengea barabara hiyo ambayo itawasaidia kuchochea shughuli za maendeleo, kukuza biashara zao ikiwemo ya utalii kwa watalii wanaopanda mlima kilimanjaro.
