Tahadhari ya kuchukua juu ya homa ya Ini


WATAALAMU wa afya wanasema ugonjwa wa Homa ya Ini huambukiza kwa njia ya virusi ambavyo vikishaingia mwilini, hushambulia ini na wanasema usipodhibitiwa mapema hugeuka kuwa ugonjwa sugu.

Wataalamu hao wanasema virusi vya ini viko katika makundi mbalimbali ambayo ni Hepatitis A, Hepatitis B, Hepatitis C na Hepatitis D.

Nimefuatilia kujua iwapo wananchi wanalifahamu hili au wanaufahamu ugonjwa huu sambamba na hatua zake. Jibu la haraka nililolipata ni hapana.

Nasema hivyo kwa sababu nimeshuhudia watu wengi wakiugua maradhi hayo bila kutambua na wanapokuja kubaini tayari muda unakuwa umeshakwenda na ugonjwa unakuwa umeshageuka kuwa tatitzo kubwa au sugu kama wanavyoainisha wataalamu wa afya. Ili wananchi waweze kujinusuru na ugonjwa huu kuna haja ya elimu kuendelea kutolewa na watoa huduma ya afya kila mara ili kujenga uelewa wa namna ya kujikinga.

Tunaambiwa ugonjwa huo unazo dalili zake lakini pia una tiba na madaktari na wataalamu wengine wa afya wana nafasi ya kutoa ushauri kwa wananchi juu ya ugonjwa huo ambao virusi vyake kitaalamu huitwa ‘Hepatitis B Virus (HBV)’. Hivi karibuni nilibahatika kuzungumza na baadhi ya madaktari, walinipa elimu na ufafanuzi juu ya ugonjwa huu, dalili, ueneaji na jinsi ya mtu anayoweza kujikinga asiweze kuugua.

Walisema virusi vya homa ya ini husambazwa kwa njia ya damu. Wanasema husambaa kwa mwingiliano wowote wa damu kutoka kwa mtu mwenye virusi kwenda kwa mtu mwingine, pia majimaji mengine ya mwilini mfano mate na jasho huweza kupitia huko na hivyo huambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kuzaliwa.

Kwa maana nyingine ugonjwa huu ukitazamwa kwa undani maambukizi yake yanawiana na ya virusi vya Ukimwi.

Hakuna asiyefahamu kuwa virusi vya Ukimwi huambukizwa kwa njia ya kushirikiana vifaa vyenye ncha kali kama nyembe, sindano na kujamiiana na mtu mwenye maambukizi bila kutumia kinga.

Hata hivyo Shirika la Afya Duniani (WHO), limetoa takwimu zinazoonyesha kuwa takriban watu milioni moja hupoteza maisha duniani kote kutokana na ugonjwa huo kwa mwaka.

Virusi kuishi nje ya mwili wa binadamu

Wataalamu wanasema kuwa ugonjwa wa homa ya ini umekuwa hatari kwa sababu una virusi vyenye uwezo wa kuishi nje ya mwili wa binadamu, wakati virusi vya Ukimwi haviwezi kuishi nje ya mwili wa binadamu hata kwa dakika moja.

Hivyo ueneaji wa virusi vya homa ya ini ni rahisi zaidi kuliko vile vya Ukimwi.

Sasa ugonjwa huu usipodhibitiwa ni hatari kwa afya ya watu.

Imefika wakati kwa wanannchi kulitafakari hili na kuanza kuchukua hatua ya kupima afya zao kila mara.

Ama wanapooina kuna dalili ya homa kali, kupungua uzito au kukosa hamu ya kula, mtu kupatwa na maumivu makali ya tumbo upande wa ini wawahi hospitali.

Dalili nyingine ni mtu kujisikia mchovu wakati wote, kupata kichefuchefu, macho, ngozi na viganja vya mikono vinakuwa vya njano.

Tunaambiwa virusi vya Hepatitis B huongezeka na kushambulia ini kiasi cha kusababisha uharibifu kabisa kwa ini.

Hata hivyo wataalamu hao wanatoa suluhisho la tatizo hilo kuwa ni kujikinga tu dhidi ya sababu za ugonjwa wa homa ya ini kwa kupata chanjo.

Kwa bahati nzuri ugonjwa huu una chanjo na mpaka sasa Hospitali ya Taifa Muhimbili inatoa.

Pia ni muhimu watu wajitokeze kujikinga kwa kuepuka kuchangia vifaa vya ncha kali kama sindano, wembe, miswaki na mavazi tumboni na maambukizi.
Mpya zaidi Nzee zaidi