Udhuru wa Kibatala wasababisha kesi ya akina Mbowe kuhairishwa


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo kwa mara nyingine imeahirisha kuanza kusikiliza maelezo ya awali ya kesi ya jinai namba 112/2018 inayowakabili Viongozi Wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na Wabunge 7.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Wilbard Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu, Agosti 13, mwaka huu, baada ya kutolewa udhuru wa kutokuwepo mahakamani hapo kwa mawakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya.

Akiwakilisha udhuru huo kwa niaba yao, Wakili Hekima Mwasipu aliiambia mahakama kuwa Wakili Kibatala yupo Mahakama Kuu mbele ya Jaji Luvanda ambako alikuwa na shauri jingine huku Wakili Mtobesya naye pia ana kesi nyingine Mahakama Kuu Mtwara.

Katika hatua nyingine, Hakimu Mkazi Mkuu Mashauri alimtaka mshtakiwa namba 5 katika kesi hiyo, Esther Matiko (Mb) kuieleza mahakama dharura iliyompata na kushindwa kuhudhuria mahakamani hapo Agosti 2, mwaka huu.

Matiko aliiambia mahakama kuwa alipigiwa simu ya dharura kutoka shuleni anaposoma mwanae wa kike, Nairobi, nchini Kenya, Agosti 1, mwaka huu hivyo akalazimika kusafiri kwa ndege ya KQ saa 4 usiku wa siku hiyo hiyo. Alipofika shuleni Agosti 2, aliambiwa mtoto wake ni mgonjwa na alipompeleka hospitali kufanyiwa uchunguzi alikutwa na ugonjwa wa Tetekuwanga.

Washtakiwa kwenye kesi hiyo ni Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe (Mb) Katibu Mkuu wa Chama, Dkt. Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu wa Chama (bara) John Mnyika (Mb), Naibu Katibu Mkuu wa Chama (Zanzibar) Salum Mwalim, Mkiti wa BAWACHA Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Halima Mdee (Mb), Mjumbe wa Kamati Kuu Peter Msigwa (Mb), Mjumbe wa Kamati Kuu John Heche (Mb), Mjumbe wa Kamati Kuu Esther Bulaya (Mb) na Mweka Hazina wa BAWACHA Esther Matiko (Mb).

Miongoni mwa mashtaka  yanayowakabili washitakiwa ni pamoja na kula njama kwa nia ya kutenda kosa, kufanya mkusanyiko usio halali, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kukiuka tamko la kutawanyika na kuendeleza mkusanyiko wenye ghasia.

Upande wa mashtaka katika hati ya mashataka iliyowasilishwa mahakamani hapi unadai kuwa washitakiwa hao kati ya Februari Mosi na 16, mwaka huu, jijini Dar es Salaam kwa pamoja na ujumla wao walikula njama ya kutenda makosa ya kufanya mkusanyiko usiokuwa halali, mkusanyiko wenye ghasia na kukiuka tamko la kutawanyika.

Inadaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu, katika Viwanja vya Buibui na Barabara ya Mwananyamala na Kawawa, Kinondoni, jijini Dar es Salaam wakiwa wamekusanyika kwa nia ya kutekeleza adhma ya pamoja ya kuandamana hivyo kuwatia hofu wananchi kwamba kutakuwa na uvunjifu wa amani.

Pia inadaiwa kuwa viongozi hao pamoja na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani, siku hiyo waliandamana isivyo halali wakiwa na lengo la kuvamia Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na kutokana na mkusanyiko huo wa ghasia walisababisha kifo cha Akwilina Akwiline na majeraha kwa  askari H. 7856PC Fikiri na E6976 CPL Rahim Msangi.
Mpya zaidi Nzee zaidi