IKIWA ni siku chache baada ya Bondia kutoka Tanzania, Hassan Mwakinyo (23), kumtwanga Bondia wa Uingereza, Sam Eggington (25) katika raundi ya pili kwa TKO, ametangaza nia ya kutaka kupambana na bondia maarufu kutoka Uingereza Amir Khan.
Pambano la Jumamosi la Mwakinyo na Eggington lilikuwa la uzito wa kati lilikuwa la utangulizi kabla ya pambano kubwa la Amir Khan dhidi ya Samuel Vargas. Khan alishinda kwa tofauti ya alama dhidi ya Vargas.
Mwakinyo aliingia katika ulingo wa Arena Birmingham, jijini Birmingham Uingereza kama mbadala wa bondia mwingine aliyetakiwa kupambana na Eggington kushindwa kufikia vigezo. Wachambuzi wengi wa masuala ya masumbwi waliliona pambano hilo kuwa rahisi kwa Eggignton ambaye alikuwa na rekodi bora zaidi lakini mambo yalimbadilikia.
Wakati Mwakinyo akiwa na rekodi ya kushinda mapambano 11 na kupigwa mawili, mpinzani wake alikuwa ameshinda mapambano 24 na kupigwa manne. Eggignton pia ni bingwa wa zamani wa Uingereza, Ulaya na nchi za Jumuiya ya Madola.
Haikuchukua muda mrefu toka pambano lianze kwa Mwakinyo kufurumushia mvua ya makonde Eggington. Mwakinyo alianza raundi ya pili kwa kasi aliyomaliza nayo raundi ya kwanza na baada ya kumsukumia makonde kadhaa bila majibu, mwamuzi wa mchezo huo Kevin Parker alilazimika kumnusuru Eggington kwa kumaliza pambano hilo.
Baada ya matokeo hayo, Mwakinyo sasa ni bondia wa 16 kati ya 1,851 duniani, pia anashikilia namba moja kati ya mabondia 11 wa Tanzania.
Mara baada ya ushindi huo, Mwakinyo alisikika akiimba kuwa anataka kupambana na bondia mwingine kutoka Uingereza, Kell Brook.
“Yeye (Eggington) aliingia ulingoni akiwa mwenye kujiamini sana. Nilitaka kuonesha uwezo wangu, sie wengine ni mabingwa pia lakini hatuonekani kutokana na mzingira tunayoishi, nimefurahi sana kwa ushindi huu na nimeionesha dunia uwezo wangu halisi,” alisema Mwakinyo baada ya pambano hilo.
“Sasa nataka kupambana na Kell Brook, na na nikishamchapa namtaka Amir Khan,” alipoulizwa kama wataweza kustahmili nguvu za Brook akajibu kwa kujiamini: “Kwani wanionaje?”
