Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, (NEC), Dk. Athuman Kihamia amekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufuta kauli waliyotoa dhidi ya tume hiyo wakidai kuwa kuna vituo hewa 15 vya kupigia kura vimeongezwa katika jimbo la Ukonga.
Kihamia amesema, wanachofanya Chadema ni kukuza maneno na kutafuta huruma ya wananchi na kutaka wafike Kamati ya Maadili ili kufikisha malalamiko yao na si kuzungumza kwenye mitandao ya kijamii.
“Jimbo la Ukonga lina vituo vya kupigia kura vilevile vilivyotumika katika uchaguzi mkuu wa 2015 na hakuna mabadiliko yoyote tuliyofanya kama tume na si Ukonga tu, majimbo yote hakuna kituo tulichoongeza labda kuhamisha kituo kutokana na sababu zilizopo kisheria”, amesema Dkt. Kihamia.
Akizungumza jijini Dar es Salaamm jana katika mkutano wake na wanahabari, Katibu Kanda ya Pwani wa CHADEMA, Casmir Mabina amesema wamefanya uchunguzi na kubaini vituo hewa vya kupigia kura ambavyo kwenye daftari la wapiga kura la mwaka 2015 havikuwepo.
‘’Tumebaini ongezeko la idadi ya vituo vya kupigia kura katika jimbo la uchaguzi Ukonga kutoka vituo 659 vilivyotumika katika uchaguzi mkuu wa 2015 hadi kufikia vituo 674 katika uchaguzi huu mdogo unaotarajiwa kufanyika Septemba 16”, amesema Mabina.
Hayo yanajiri ikiwa zimesalia siku tano pekee kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa wabunge na madiwani katika majimbo ya Ukonga jijini Dar es salaam, Korogwe Vijijini mkoani Tanga pamoja na Monduli jijini Arusha.
