Faru kufungwa vifaa kuwalinda wasitoweke


NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, amesema kukua kwa teknolojia ya kisasa kutawasaidia maofisa wanyamapori kuwa na uwezo wa kuwaona faru popote walipo wakati wakiwa wamekaa ofisini, hali itakayosaidia kuwalinda na hatari ya kuuawa na majangili.

Alisema maofisa hao watakuwa na uwezo wa kufuatilia mienendo ya wanyama hao popote wanapoenda, ili kujua kama wanaumwa au wana tatizo lolote hali itakayosaidia kwenda kutoa huduma ili wanyama hao waendelee kuishi.

Alisema hayo alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti baada ya kushuhudia uwekaji wa vifaa vya utambuzi kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa faru waliopo katika hifadhi hiyo.

Alisema hatua hiyo ni muhimu kwenye uhifadhi wa wanyamapori na itasaidia majangili kukamatwa kabla ya kumuua mnyama.

Mratibu wa Mradi wa Faru katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Phillibert Ngoti, amemweleza Naibu Waziri huyo kuwa uwekaji alama za vifaa vya kisasa unafanywa katika hifadhi hiyo kwa kushirikina na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Frunkfurt Zoological Society (FZS) pamoja Friedkin Conservation Fund (FCF).

Alifafanua kuwa uwekaji wa vitambuzi hivyo unafanyika kwa namna mbili, vitambuzi vinavyowekwa ndani ya pembe za faru na vinavyowekwa kwenye mguu mmoja wa mbele wa faru ili kusaidia kujua popote pale walipo.

Kiongozi wa Mradi wa Uhifadhi kutoka FZS, Rian Habuschagne, alisema mradi huo umefadhiliwa na Frunkfurt Zoological Society kwa kushirikiana na Friedkin Conservation Society.

Alisema wamesaidia helikopta, mahema, kumlipa rubani, chakula kwa askari wanyamapori pamoja na magari na hadi kukamilika kwa mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Shilingi bilioni moja.

Alisema utaratibu wa uwekaji vitambuzi kwa faru umekuwa pia ukifanyika nchini Afrika Kusini hali iliyosaidia kuwalinda faru.

Aidha, Daktari wa Wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Alex Muse, anayeshiriki uwekaji vitambuzi kwa faru, alisema kazi hiyo ina changamoto, lakini kwa kusaidiana na timu yake, inakwenda vizuri.

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items