Mbowe agoma kung'atuka, awataja watakaomvua Uenyekiti Chadema


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe amesema hatokuja kuipigia magoti CCM na kusema hatong'atuka katika nafasi yake ya uenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani.

Mbowe amesema amekuwa akisikia kelele nyingi kutoka kwa makada na viongozi wa CCM kuhoji uwepo wake kwenye nafasi hiyo ya juu ya uongozi ndani ya Chama na kusisitiza ataondoka iwapo wanachama waliomchagua kikatiba wataona inatosha kwa yeye kuhudumu kwenye nafasi hiyo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wandishi wa habari makao makuu ya chama hicho kuelezea msimamo wao wa kutoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kutokana na kufanyiwa rafu nyingi kwenye uchaguzi wa Ukonga na Monduli.

" Siwezi kuinyenyekea CCM hata siku moja, sitowapigia magoti, wao furaha yao ni kuona Mbowe anakua dhaifu na siyo mwenye nguvu maana hawatutakii mema hata kidogo, ndiyo maana wanapigia kelele nafasi yangu ya uenyekiti," amesema Mbowe.