Mbunge aibuka na suala la vyeti feki

MBUNGE wa Viti Maalum (Chadema), Aida Khenani, amehoji mkakati wa serikali wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na watumishi waliokumbwa na sakata la vyeti feki.

Akiuliza swali bungeni jana, mbunge huyo alisema kabla ya mchakato wa kuondoa watu wa vyeti feki kulikuwa na upungufu mkubwa wa watumishi ikiwamo sekta ya elimu, kilimo na afya.

"Kwa kuwa kulikuwa na upungufu na mkaongeza upungufu mkubwa zaidi, mpaka sasa kuna upungufu wa watumishi kiasi gani?” Alihoji.

Aidha, alihoji serikali ina mpango gani wa kuwalipa mafao yao watumishi hao.

Akijibu maswali hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika, alisema serikali ilishatoa kibali cha kuajiri watumishi wapya 15,000 ili kuziba pengo lililosababishwa na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti.

Alisema vibali vya kuajiri watumishi hao vimetolewa katika ngazi ya Wizara, Idara zinazojitegemea, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa na waajiri wote wameendele kujaza nafasi hizo.

"Serikali pia imetoa vibali vya ajira kwa mamlaka zote za serikali za mitaa kumb.Na.CFC.26/205/01/PF/91 cha tarehe 22 Agosti 2017 na kibali Kumb.Na.CFC.26/205/01/GG/95 cha tarehe 12 Machi, 2018 kuziba nafasi zote za watendaji wa vijiji na mitaa zilizoachwa wazi kutokana na zoezi la kuhakikiwa vyeti," alisema.

Kadhalika, alisema katika mwaka wa fedha 2017/18 kwa kutambua umuhimu wa kuajiri watumishi wa kada mbalimbali serikali imetoa vibali vya kuajiri watumishi 22,150.

Alisema watumishi hao ni pamoja na wa kada ya ualimu 6,840, fundi sanifu wa maabara za shule 160, kada ya afya 8,000, wahadhiri wa vyuo vikuu 624 na watumishi wa kada zingine ni 6,526.

Kuhusu kulipwa mafao, alisema serikali haiwezi kuwalipa kwa kuwa walipeleka vyeti feki, hivyo mkataba unakuwa umefutika kutokana na kuwasilisha taarifa za uongo.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items