NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Vijana, Kazi na Ajira), Anthony Mavunde, amesema sheria za nchi hazijaruhusu uraia pacha na hakuna watu maalum waliopewa uraia wa aina hiyo.
Mavunde alisema hayo wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali aliyetaka kujua kumekuwa na raia wengi kutoka Msumbiji katika jimbo la Mchinga hasa vijiji vya Kilangala B, Butamba, Mvuleni, Kitolambwani na Kikonde wamekuwa wakishiriki chaguzi katika nchi zote yaani Tanzania na Msumbiji.
"Je, serikali imepitisha utaratibu wa raia pacha na kuwapa watu maalum? Pia Raia hao ni Watanzania au wa Msumbiji?” Alihoji.
Mavunde alisema kwa mujibu wa ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi nchini.
Alieleza Ibara ya 5 (2) (a) ya katiba hairuhusu mtu mwenye uraia wa nchi nyingine kushiriki katika shughuli za uchaguzi ikiwamo kupiga kura.
"Ili mtu aweze kupiga kura lazima awe ameandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapigakura lililoanzishwa chini ya ibara ya 5(3)(a) ya Katiba na uandikishaji wa wapiga kura unapokamilika daftari la awali huwekwa wazi kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343 ili kukaguliwa na wananchi," alisema.
Kadhalika, alisema kifungu cha 24 (1) cha sheria hiyo kinatoa fursa kwa mtu ambaye kajiandikisha kuweka pingamizi dhidi ya mtu mwingine aliyeandikishwa kwenye daftari ikiwa amebainika kuwa hana sifa ya kuandikishwa kwa kutokuwa raia wa Tanzania.
