Aliondoka Adolf Hitler sasa tunasema 'Auf Wiedersehen Deutchland'


Na Tom Thomas
Jioni ya Mei Mosi mwaka 1945, mtangazaji Karl Lehmann alitangaza habari iliyoleta furaha duniani kote. Alitangaza kifo cha Dikteta mkatili, Adolf Hitler. Ndio, ilikua habari iliyofurahiwa na kila mtu aliyeisikia. Kwa takribani miaka miaka sita dunia ilikua katika vita. Vita ya pili ya dunia ambayo ilianza September 21, 1939.

Chanzo kikubwa cha vita hii ni utawala wa kidikteta wa mjerumani Adolf Hitler na chama chake cha Nazi. Hitler alihitaji kuifanya Ujerumani kuwa Taifa kubwa zaidi duniani.

Hakutaka kuwa chini, alihitaji kuwa na mamlaka makubwa kwa mataifa yote.

Alichokifanya kwanza ni kuondoa muundo wa kidemokrasia ili Ujerumani iwe chini ya chama kimoja, chama chake cha Nazi. Kisha akaifanya kuwa nchi ya kidikteta.

Baadaye akatamani kutawala nchi nyingi zaidi. Ili kufanya hivyo ilimlazimu apigane vita. Ikawa hivyo. Vita ikaanza, ikizihusisha karibu nchi zote duniani.

Adolf Hitler anatajwa kuwa binadamu mkatili kuwahi kutokea duniani. Ameua zaidi ya watu milioni 20 kwa amri yake. Ni idadi kubwa sana ya watu. Hakua na huruma. Alichokihataji siku zote ni kuona malengo yake yakitimia.

Bahati mbaya alishindwa. Baada ya miaka sita ya vita aliondoka duniani. Inasadikika alijiua yeye pamoja na mke wake. Habari ya kifo chake ikafurahiwa na kila mtu. Huo ndio ukawa mwisho wa vita kuu ya pili ya dunia. Weka pini hapa!

Baada ya miaka mingi kupita, wajerumani walitamani kuendeleza kile Adolf Hitler alichokianzisha. Wakati huu ilikua ni tofauti kidogo. Walihitaji kutawala soka duniani. Walitamani kuiona timu yao ya taifa ikizifunga timu zote inazokutana nazo.

Kwa miaka mingi wamefanikiwa katika hili, wameendelea kuwa bora. Wakiwa na kikosi chenye wachezaji mahiri. Wakishinda mataji. Wameshinda ubingwa wa dunia mara nne sawa na Italy, wakiwa nyuma ya Brazil ambao wameshinda mara tano.

Fainali ya mwaka 1954 mjini Bern ndiyo iliyofungua njia ya soka la Ujerumani. Wao wanaiita 'Wunder von Bern' wakimaanisha muujiza wa Bern. Hawakuamini kilichotokea siku hiyo. Waliona ni maajabu.

Walitoka nyuma ya magoli mawili na kufunga magoli matatu dhidi ya Hungary, timu iliyokua bora sana wakati huo. Hungary ya mbabe Ferenc Puskas. Wakashinda ubingwa wa kwanza wa dunia.

Utawala wao ulianza hapa. Wakatamani kushinda zaidi na zaidi ni kama vile Adolf Hitler alivyokua akitamani kushinda kila vita. Brazil ndiyo taifa lililokua likiwapa changamoto mara nyingi.

Wabrazil wanaamini mpira ni asili yao, mpira ulizaliwa kwao. Ndivyo ilivyokua, walipambana sana kuhakikisha utawala wao wa soka hauchukuliwi na Wajerumani.

Kwa sasa kizazi chao bora kinaondoka. Kinaondoka bila ya kufanikiwa kulitawala soka la duniani. Ni kama vile Adolf Hitler alivyoondoka bila kutimiza lengo lake. Bahati mbaya sana hii.

Kizazi kilichoshinda ubingwa wa dunia miaka minne iliyopita hakipo tena. Hayupo Bastian Shweinstaiger, hawapo kina Phillip Lahm, Mesut Ozil, Miroslav Klose, Benedikt Höwedes, Per Mertasacker na Andre Schurrle.

Hata yule mfungaji wa goli la fainali, Mario Gotze hayupo. Hawa wanaendelea kucheza hadi sasa kina Matts Hummels, Sami Khedira, Jerome Boateng na Thomas Muller makali yao hayapo tena. Wana muda mchache wa kucheza kabla ya kustaafu.

Ni wazi sasa soka la Ujerumani tunaliaga taratibu. Timu yao imeshinda mechi moja kati ya tano zilizopita. Mwanzoni walijaribu kutafuta nani mchawi anayewafelisha waakahisi pengine ni Mesut Ozil.

Ilikua ni Ozil kwa sababu wamekua na historia ya kuwa na wachezaji wapambanaji, wenye roho ya kijerumani halisi tangu enzi za kina Franz Beckenbauer, Andreas Brehme, Gerd Muller, Paul Breitner, Lothar Mathaus, Michael Ballack na Oliver Kahn.

Ozil akatengenezewa lawama nyingi kwamba si mchezaji mpambanaji uwanjani, kwamba hana uzalendo kwa taifa lake. Hawakujua!

Hawakujua kwamba, timu yao ina matatizo mengi kwa sasa. Hawakuona jinsi kizazi chao bora kinavyozidi kuondoka. Hawakujua kwamba hawa wachezaji wao vijana bado wanahitaji muda wa kujifunza mengi zaidi.

Hawakujua kwamba Bayern Munich ambayo imekua na muhimili mkubwa wa kutoa wachezaji wengi wanaokuja kufanya vizuri timu yao ya taifa kwa sasa haiko hivyo tena. Kikosi chao cha kwanza kinaweza jumuisha wachezaji watatu tu wa Kijerumani.

Hata wale Wajerumani halisi kina Michael Ballack, Bastian Shweinsteiger na Phillip Lahm hawapo tena. Waliopo ni hawa machotara kina Emre Can, Niklas Sule, Thilo Kehrer, Serge Gnabry na Leroy Sane.

Nilikiangalia kikosi kilichoanza mechi iliyopita dhidi ya Ufaransa. Kilikua na wachezaji watatu tu walioshinda ubingwa wa dunia miaka minne iliyopita. Ni kikosi kipya, chenye wachezaji wengi vijana.

Pengine ni tofauti na miaka iliyopita safari hii watahitaji muda zaidi kukitengeneza kikosi hiki cha vijana kitakacho jaribu kuyafikia mafanikio ya Brazil na kutawala soka la dunia.


Kilipoondoka kizazi cha kina Fritz Walter kikaja cha kina Gerd Muller na Franz Beckenbauer.  Baadaye kikaja cha kina Andres Brehme, Mattias Sammer, Juergen Klinsmann na Lothar Matheus kisha kina Oliver Kahn na Michael Ballack wakaja. Cha mwisho ni hiki cha kina Toni Kroos kilichobaki wa wachezaji wachache.

Kizazi cha sasa na kijacho ni hiki kisichoeleweka. Chenye wachezaji kama Joshua Kimmich, Leon Goretzka, Timo Werner na Julian Brandt. Joachim Low anaweza kupoteza kazi kwani kizazi hiki kinafeli.

June mwaka jana alikwenda Russia kushiriki mashindano ya kombe la mabara akiwa na kikosi hiki. Alishinda ubingwa kwa kuifunga Chile isiyoeleweka. Ikaonekana Wajerumani bado wana jeuri ya kutawala soka kwa miaka mingi ijayo bila kujua kilikua ni kikosi dhaifu kinachokosa wapambanaji.

Waliporudi Russia, wakauona udhaifu wa kikosi chao. Hawaamini kinachoendelea hadi sasa. Wengine wanadhani ni muda wa Low kuondoka, wengine wanabaki kuwalaumu wachezaji. Hawaelewi nini cha kufanya.

Alikuja mkatili Adolf Hitler akataka kuitawala dunia akashindwa. Akaondoka. Sasa kizazi cha wakatili wajerumani kilichoiadhibu Brazil goli saba tena kwenye ardhi yao ya nyumbani kinaondoka bila kutawala soka la dunia.

'Auf Wiedersehen Deutchland' ni maneno ya lugha ya kijerumani yenye maana, kwaheri Ujerumani. Ni muda wa kuwapa mkono wa kwaheri wajerumani.

0754 896 963