Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imesitisha leseni za usafirishaji abiria kwa siku 30 kwa mabasi manne yanayofanya safari zake mikoani.
Mamlaka hiyo imesema imechukua uamuzi huo baada ya wahusika kubainika kuingilia mfumo wa kufuatilia mwendokasi wa mabasi (VTS).
Magari hayo ni Tahmeed Coach, magari mawili ya kampuni ya Off Road Express na gari moja linalomilikiwa na kampuni ya Frester Investment Ltd.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabarani wa Sumatra, Johansen Kahatano, alisema magari hayo yalibainika kuchezea mfumo wa VTS, hivyo yamesitishiwa leseni zao kwa muda.
“Zoezi la ukaguzi ni endelevu haliishi, tunaendelea kuyafuatilia magari yote na Mamlaka inaendelea kuchukua hatua kwa wasafirishaji wanaokiuka masharti ya leseni za usafirishaji na itachukua hatua kali zaidi kwa wale wanaofanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara,” alisema Kahatano.
Kahatano alisema kumekuwa na vitendo vya madereva wa mabasi yaendayo mikoani kuchezea mfumo wa VTS na amewataka kuacha mara moja tabia hiyo.
Alipoulizwa endapo Sumatra imetoa adhabu nyingine kwa mabasi waliyoyakamata mbali na kuyasitishia leseni, Kahatano alisema kwa mujibu wa sheria kosa walilofanya adhabu ni kusitishiwa leseni kwa siku 30, kisha kurudishiwa baada ya kipindi hicho.
Alisema Sumatra wamefunga mfumo wa VTS katika magari yote yaendayo mikoani na wanayafuatilia hivyo endapo dereva akichezea mfumo huo ni rahisi kubainika.
Aidha, Kahatano aliwasihi wamiliki wa mabasi hayo kuwa na tabia ya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa magari yao, kwani endapo yakibainika na makosa adhabu itayahusu mabasi yao.
Hatua ya Sumatra kufunga mfumo huo, inatokana na ajali za mara kwa mara za barabarani zinazosababishwa na mabasi yanayokwenda mkoani kutokana na madereva wake kuendesha mwendo kazi.
Ajali hiyo zimesababisha vifo vya watu wengi na uharibifu wa mali.
