Na John Walter-Babati
Mamlaka ya maji na usafi wa Mazingira mjini Babati [BAWASA] imetenga kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya usambazaji wa maji katika maeneo ambayo hayana huduma ya maji safi na salama.
Aidha Mamlaka hiyo imeiomba serikali shilingi Bilioni 2.7 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji mtaa wa Kwere juu na Bonga.
Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka hiyo Iddy Yazid Msuya ameiambia Muungwana Blog kuwa Mitaa ya Ngw’angw’aray ambao wanatumia maji yasiyotibiwa pamoja na Nangara juu wameshapatikana wakandarasi wa kufanya kazi ya kwapelekea maji baada ya kutangaza Zabuni na wanatarajia kuikamilisha kazi hiyo February 2019.
Eng. Msuya amesema kwa sasa BAWASA inafanya jitihada za kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya miinuko ambayo ni Kwere Juu pamoja na kata ya Mutuka.
Mamlaka ya maji na usafi wa Mazingira mjini Babati [BAWASA] Ilianza 13.12 mwaka 2002 ikiwa na mtandao wa maji Kilomita 12, wateja 925 ambapo imepiga hatua kubwa hadi kufikisha wateja zaidi ya 7890 mwaka 2018.
Hadi sasa mji wa Babati unapata huduma ya maji kwa asilimia 75% bado asilimia 20% ili kufikisha malengo ya asilimia 95% ifikapo mwaka 2020 ikiwa ni malengo ya serikali.
Pamoja na hayo Mkurugenzi wa Bawasa amewaomba wakazi wa Babati kuendelea kushirikiana na Bawasa kwa kutoa taarifa wanapoona upotevu wa maji na kutunza vyanzo vya maji.
