Chakula huimarisha mahusiano mazuri ya familia

Familia bora ni ile ambayo inayoishi kwa upendo na amani, lakini ili ubora huo utimie wanafamilia wanahitaji muda wa kukaa pamoja na kuzungumza mustakabali wa maisha yao.

Familia inayotajwa hapa inajumuisha wazazi yaani baba na mama, pia watoto ambao wamejaariwa kuwa nao. Lakini kutokana na shughuli nyingi wana familia wanakosa muda wa kukutana pamoja.

Muda wa kukutana kwa wanafamilia ni muda maalumu ambao hauingiliani na shughuli nyingine yoyote.  Kutokana na kukosa muda wa kukutana na watu wetu wa karibu tunajikuta  tunafanya kazi kwa bidii lakini tunakosa furaha.

Kutokana na shughuli nyingi ambazo tunakuwa nazo kila siku, muda mzuri wa kukutana ni wakati chakula. Lakini sio familia zote ambazo hupata chakula pamoja.

Tafiti zinaonyesha kuwa familia ambazo zinakula chakula pamoja zinapata  faida nyingi. Kula pamoja kunaimarisha mawasiliano na mahusiano ya watoto na wazazi. Watoto ambao wanakula chakula pamoja na wazazi wana nafasi nzuri ya kufanya vizuri katika masomo yao na kufanya maamuzi sahihi katika maisha yao na kuhimili ushawishi wa makundi rika, unywaji wa pombe, matumizi ya dawa za kulevya na ngono. Pia wanajifunza jinsi ya kula mlo kamili tangu wakiwa wadogo mpaka wakifikia umri wa kujitegemea.

Huenda ni vigumu kula chakula pamoja na familia yako kwasababu ya mazoea uliyonayo ya kula ukiwa peke yako, fuata njia zifuatazo kukusaidia kupata chakula cha jioni na familia yako ili kuimarisha mahusiano:

Wape uhuru wa kuchagua
Kama ni mzazi wape uhuru wana familia kuchagua chakula ambacho wangependa kula. Ukiwaruhusu watajisikia wanawajibika na wana maamuzi katika masuala muhimu ya familia.

Tengeneza ratiba ya Chakula
Kuwa na ratiba ya chakula ambayo inaainisha aina ya chakula ambacho familia inatarajia kula kila siku ni jambo jema. Watoto wanapenda mambo yaliyo kwenye mpangilio mzuri, kupitia njia hiyo unawajengea uwezo wa kufuata na kuheshimu ratiba kwa kila jambo wanalolifanya. 

Gawa Majukumu
Kila mmoja ana nafasi ya kushiriki kuandaa chakula cha familia. Kama mzazi mpe majukumu kila mtu katika familia, mwingine anaweza kuandaa meza ya chakula, kuosha vyombo, ili mlo ukamilike utagundua kila mtu anawajibika kwa namna moja au nyingine. Maamuzi hayo yatasaidia kuimarisha uhusiano na watoto kufahamu majukumu yao.

Zingatia Muda
Ni  vema muda wa kula ukapangwa ili wana familia wote wafahamu wakati sahihi wa wao kukutana mezani kwa ajili chakula. Watoto watafaidika kwa kujifunza umuhimu wa kuzingatia muda kwa kila jambo wanalofanya.

Ongeza vionjo vingine
Chakula kinapaswa kifurahiwe, ukiweka vionjo vya muziki, mazungumzo ya kufurahisha vyote vinaongeza hamasa ya wana familia kushiriki kikamilifu katika meza ya chakula. Huu sio wakati wa kuibua mambo mabaya au kauli za kuudhi ambazo zinalenga kumtenga mtu.  Kila jambo na wakati wake.

Hata hivyo, hizi ni baadhi ya njia za kuimarisha mahusiano katika familia, lakini kila familia ina taratibu za kuendesha mambo yake na kujenga mstakabali mzuri.