Na John Walter-Babati
Katika hali isiyo ya kawaida, mama mmoja mkazi wa Kijiji cha
Diffir, Kata ya Ufana, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, amejifungua mtoto wa
kiume bila mikono wala miguu katika Kituo cha Afya Bashnet.
Mtoto huyo alizaliwa Februari 9, 2026 siku ya Jumatatu
majira ya saa tano usiku kwa njia ya kawaida, akiwa na uzito wa kilo 2.3.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya
Babati, Dkt. Madama Hosea, licha ya kuzaliwa bila viungo hivyo, mtoto alikuwa
mzima na hakuwa na changamoto nyingine za kimaumbile wakati wa kuzaliwa.
Mtoto huyo alikuwa ni uzao wa 12 katika familia hiyo, ambapo
wa kike ni wanne na wa kiume ni wanane akiwemo yeye.
Mama wa mtoto huyo ana umri wa miaka 47 na hakuwa mtumiaji
wa pombe wala sigara wakati wa ujauzito.
Dkt. Madama, aliyeongoza timu ya wataalamu wa afya kufika
katika kituo hicho kufuatilia tukio hilo, alisema kuwa katika kipindi chake cha
miaka 15 ya utumishi kama daktari hajawahi kukutana na tukio la aina hiyo.
Aidha, alieleza kuwa matumizi ya pombe na tumbaku kwa mama
mjamzito, hasa katika miezi mitatu ya mwanzo wa ujauzito, yanaweza kusababisha
changamoto za kimaumbile kwa mtoto. Hata hivyo, katika tukio hili, mama huyo
hakuwa na historia ya matumizi ya vitu hivyo.
Kwa masikitiko, mtoto huyo alifariki dunia Februari 11, 2026
siku ya Jumatano majira ya saa tano usiku, baada ya kupata degedege kali.
Awali mama alionekana kutaharuki, lakini yeye na mume wake
walikubali hali hiyo kwa moyo wa subira.
Amesema kuwa kama mtoto wao asingefariki, wangemlea kama
mtoto mwingine yeyote.
Dkt. Madama ametoa wito kwa kina mama wajawazito kuhakikisha
wanahudhuria kliniki zote nane kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya, pamoja
na kutumia dawa za madini ya chuma na virutubisho vingine wanavyopewa ili
kulinda afya zao na za watoto wao.
Ameongeza kuwa Kituo cha Afya Bashnet, kilichojengwa kwa
mapato ya ndani kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 600, kimeendelea kuwa
mkombozi mkubwa wa huduma za afya katika Kanda ya Bashnet na maeneo ya jirani.
Licha ya changamoto hiyo, familia imesema mtoto huyo alikuwa
ni zawadi kutoka kwa Mungu, na wamepokea yote yaliyotokea kwa imani na utulivu.

0 Maoni