F TANESCO Hanang Yapokea Gari Jipya la Kisasa Kuimarisha Huduma za Umeme | Muungwana BLOG

TANESCO Hanang Yapokea Gari Jipya la Kisasa Kuimarisha Huduma za Umeme





Na John Walter -Hanang'

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara limepokea gari jipya aina ya Isuzu FRR lenye mitambo ya kisasa kwa ajili ya kuboresha huduma za umeme wilayani humo.

Gari hilo limekabidhiwa leo rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Almish Hazal, katika hafla iliyofanyika kwenye ofisi za TANESCO Hanang’.

 Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Hazal amesema gari hilo lina uwezo mkubwa wa kubeba vifaa vizito, kubadilisha nguzo pamoja na transfoma kwa urahisi, hivyo litasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya TANESCO.

Hazal amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mafanikio ya serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za umeme, akieleza kuwa vijiji vyote 96 vya Wilaya ya Hanang’ tayari vimepata umeme, na sasa juhudi zinaelekezwa kwenye vitongoji 116 vilivyopo katika kata 33 za wilaya hiyo.

“Gari hili litasaidia sana utendaji kazi wa TANESCO, hasa kuwafikia wananchi kwa haraka pale changamoto za umeme zinapotokea,” amesema Hazal.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANESCO Wilaya ya Hanang’, Mhandisi Mwitondi Charles Rugembe, amesema kabla ya kupatikana kwa gari hilo walilazimika kukodi gari kwa gharama kubwa, hali iliyoongeza matumizi yasiyo ya lazima.

“Awali tulikuwa tunakodi gari na kutumia gharama kubwa, lakini sasa serikali imeokoa fedha hizo kupitia upatikanaji wa gari hili jipya,” amesema Rugembe.

Ameongeza kuwa gari hilo litasaidia kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, kwani sasa wataalamu wataweza kufika kwa wakati kwenye maeneo yenye hitilafu na kufanya matengenezo haraka.

Naye Mbunge wa Jimbo la Hanang’, Asia Halamga, amesema kuwa TANESCO wilayani humo tayari imepata gari la kutembelea pamoja na gari hilo jipya la kazi nzito, jambo linaloonesha dhamira ya serikali katika kuboresha miundombinu ya huduma za umeme.

Asia amewataka wananchi kuendelea kumuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kupeleka miradi zaidi ya maendeleo katika Wilaya ya Hanang’.


Chapisha Maoni

0 Maoni