Lukuvi aiagiza Tanesco iwalipe wanakijiji 14 fidia zao haraka

 Na John Walter-Babati

Waziri wa ardhi Nyumba na maendeleo ya makazi william Lukuvi ameliagiza shirika la umeme TANESCO kuwalipa fidia wanazodai  wananchi 14 waliojenga katika shamba la Endasago lililopo kijiji cha Dudiye kata ya Ari wilayani Babati unapopita mradi mkubwa wa umeme Kilowat 400.

Ameagiza watu hao walipwe  kuanzia leo ijumaa Novemba 23 ili wahame katika maeneo hayo na kupisha mradi uendelee.

Uamuzi wa kulipa fidia kwa wananchi hao unatoa suluhu ya muda mrefu baina ya mmiliki wa shamba kampuni ya Endasago co ltd na wananchi waliojenga katika njia ya kupitisha umeme wa mkongo kutoka Singida kupitia Babati, Namanga mpaka Kenya huku utata ukiwa ni nani anastahili kulipwa fidia kati ya pande hizo mbili.

Amelitaka shirika la Umeme tanesco kuendelea na zoezi la kuweka nguzo kwa ajili ya kukamilisha upitishaji nyaya za umeme katika mashamba yote mawili ya Endasago na Singu lakini malipo ya fidia yatakuwa kwa wale wananchi wa kijiji cha Endasago pekee.

“Tanesco muendelee na uwekaji nguzo katika mashamba yote mawili na wananchi wasimame kufanya shughuli yoyote wakati wa zoezi hilo.

Pamoja na uamuzi wa fidia, Lukuvi ameitaka halmashauri ya wilaya ya Babati kupima upya eneo la shamba la Endasago na kumpatia  mmiliki wake  eneo kulingana na mahitaji yake. Aidha, alimuagiza mmoja wa wana hisa wa Kampuni ya Endasago Abraham Mchinja kufuatilia hati ya shamba pamoja na kuhuisha umiliki wa kampuni ya Endasago co Ltd ambayo wanahisa wake wawili wamefariki dunia na kubaki mmoja pekee.

Mbunge wa jimbo la Babati Paulina Gekul aliiomba serikali kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi wa vijiji vya Endasago na Singu dhidi ya wamiliki wa mashamba hayo mawili kwa kuwa wananchi wa vijiji hivyo wamekuwa wakiishi eneo hilo kwa muda.

Kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro mkubwa baina ya wananchi wa vijiji vya Singu, Sigino na Daglailoy vilivyopo kata ya Singu na vile vya Endasago na Dudiye vilivyopo kata ya Ari wilayani Babati na wamiliki wa mashamba ya Endasago lenye ukubwa wa  1300 na Singu ekari 3013 kuhusiana na umiliki wa mashamba.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items