Machinga watakiwa kufanya biashara maeneo rasmi yaliyoruhusiwa


Wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga) katika Jiji la Dodoma wametakiwa kufanya biashara zao kwenye maeneo rasmi yaliyoruhusiwa na jiji, ili waweze kutambuliwa kwenye vikundi na kupatiwa mikopo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma, alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara hao kwenye maeneo mbalimbali ya jiji.

Katika ziara hiyo, Mavunde aliambatana na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi, kwa lengo la kuwatembelea wafanyabiashara hao mguu kwa mguu, mitaani ili kujua changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.

Akizungumza nao, Mavunde aliwataka kufanya biashara zao kwenye maeneo rasmi yaliyotengwa na jiji ili waweze kutambuliwa na kupata fursa mbalimbali ikiwamo mikopo ya kukuza biashara zao.

Aidha, alisema kwa sasa kuna ujenzi wa soko kubwa la kisasa eneo la Nzuguni ambalo litakuwa na nafasi ya kutosha kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo, bodaboda, bajaji na magari makubwa hivyo wavute subira wakati serikali inakamilisha ujenzi huo.

Kwa upande wake, Kunambi aliwaagiza kinamama wanaouza mboga katika maeneo mbalimbali ya jiji kuacha kupanga bidhaa zao chini kwa sababu ni kinyume ya taratibu za kiafya.

"Maeneo haya sio ya biashara kwa hiyo haturuhusu mtu kujenga wala kuning'iniza kamba au kuweka mabanzi katika maeneo haya, kama unahitaji kufanya hivyo basi hakikisha unaondoka na vifaa vyako vya biashara ili kuacha mazingira yetu kuwa safi," alisema Kunambi.

Hata hivyo, alimwagiza Ofisa Masoko wa Jiji la Dodoma, James Yuna, kushirikiana na viongozi wa machinga ili kupata maeneo mapya na rafiki kwa ajili ya wafanyabiashara hao.

Aidha, aliwaasa wamachinga hao kujifanyia tathmini ya mara kwa mara ili waweze kukua na kufungua maduka makubwa badala ya kuendelea na kuwa machinga miaka yote.

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items