SERIKALI imesema imeanza kuyafanyia kazi kimya kimya mashirika yote yasiyo ya kiserikali ambayo yameshindwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii, Dk. John Jingu, ndiye aliyesema hayo na kufafanua zaidi kuwa NGO itakayobainika kwenda kinyume itachukuliwa hatua, ikiwamo kufutiwa usajili
“Tayari tumeanza kuzifanyia kazi kimya kimya NGO zote ambazo zimeshindwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kwa sababu mtu hasipotii sheria, sisi tutatumia shuruti na tutashughulika nao kimya kimya,” aliongeza Dk. Jingu.
Alionya kuwa shirika lolote litachukuliwa hatua kali, ikiwa litashindwa kufanya kazi kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya NGO ya Mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa marekebisho 2005.
Akizungumza na Wasajili Wasaidizi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Arusha, Dk. Jingu alisema, kanuni mpya za sheria ya NGO zinataka mashirika hayo kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji.
Aliwaambia wasajili hao kuwa misingi ya uwazi na uwajibikaji kama inavyobainishwa katika sheria hiyo, imekuja kufuatia haja ya serikali kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Kufuatia hali hiyo, Dk. Jingu alionya pia NGO yoyote itakayobainika kufanya kazi bila kufuata katiba yake, itakosa sifa na kufutiwa usajili kwa kanuni ya sheria ya NGO ya 2002, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005, ambayo inazitaka NGO kufanya kazi kama ilivyobainishwa katika katiba ya shirika husika.
Aliwataka wasajili hao kusimamia NGO katika maeneo yao kwa kuzingatia yale yaliyobainishwa katika kanuni za sheria ya NGO na kuwataka kuwasiliana na Ofisi ya Msajili kila wakati kwa lengo la kupata usaidizi ikiwa kutakuwa na jambo lolote linalowatatiza.
Aidha Dk. Jingu aliwaambia wasajili wasaidizi kuwa makini, kwa kuwa baadhi ya mashirika yanashiriki katika vitendo viovu, akiyataja baadhi kujihusisha na vitendo vya utakatishaji fedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali, Neema Mwanga, aliwataka wasajili hao kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, vinginevyo atakayebainika kufumbia maovu ya mashirika atamwondoa katika nafasi hiyo na kukabidhi jukumu hilo kwa ofisa mwingine hata kama hatakuwa na taaluma ya maendeleo ya jamii.
Alitoa onyo hilo wakati akitoa mada ya kanuni za sheria ya NGO ya 2002 kama ilivyofanyiwa marekebisho 2005 na kuwakumbusha wajibu wao katika kusimamia NGO kwa lengo la kuwakumbusha mabadiliko ya sheria, ili wafanye kazi kwa mujibu wa kanuni mpya.
