Serikali imesema kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu inawajibu wa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuandaa,kusambaza na kutumia takwimu rasmi na bora ili kuweza kukabiliana na changamoto za kitakwimu walizonazo.
Akizungumza jijini Dodoma Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji ,wakati wa maazimisho ya siku ya Takwimu Afrika ambapo amesema kuna madhaifu makubwa katika halmashauri ambayo yanapelekea kutekeleza program na miradi mingi ya maendeleo kwa kiwango cha chini.
Hata hivyo Dkt.Kijaji amesema kuwa Serikali haiwezi kuboresha huduma za jamii kama jamii husika haijui umuhimu wa takwimu katika kupanga,kutekeleza, kufuatilia na kusimamia program na miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao.
Dkt.Kijaji amesema kuwa kuna changamoto nyingi za upotoshaji unaofanywa na watu na taasisi mbalimbali hapa nchini,nakusema kuwa sheria ya takwimu ya mwaka 2015 na kanuni zake imebainisha utaratibu wa kuandaa na kusambaza takwimu rasmi na bora.
“Ni jukumu la Ofisi ya Taifa ya Takwimu kutoa elimu kwa umma kuhusu athari na madhara ya kupotosha takwimu,mbalimbali na kutoa elimu pia mnapaswa kukemea na kuchukua hatua dhidi ya wale wote wanao potosha umma kwa makusudi au kwa kutumiwa na taasisi au watu wenye maslahi binafsi”amesema Ashatu.
Dkt.Kijaji amesema kuwa kifungu cha 24B (1) kinakataza mtu kutoa taarifa za kitakwimu zenye lengo la kupotosha umma pamoja na adhabu inayostahili kutolewa kwa yeyote atakaye fanya hivyo,mmepewa mamlaka haya kisheria hivyo simamieni sheria kwa maslahi mapana ya taifa letu na si vinginevyo.
Aidha amesema kuwa changamoto nyingine ni kukosekana kwa kada ya takwimu katika muundo wa serikali na taasisi zake kwani hakuna idara wala Ikama ya kada ya takwimu katika Wizara,Idara zinazojitegemea, Wakala,Mashirika na Mamlaka za serikali za mitaa.
“Madhaifu mengi ya kitakwimu mahala pa kazi yanatokana na kada hii ya takwimu kupewa hadhi ndogo ikilinganishwa na umuhimu wake,hivyo basi kama taifa tunapaswa kujitathimini kuhusu ombi la kada ya Takwimu katika muundo wa serikali na taasisi zake”amesema Dkt.Kijaji
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali Ofisi ya Taifa ya Takwimu Albina Chuwa amesema kuwa lengo kuu la kuasisi maadhimisho hayo ni kuelimisha umma katika bara la Afrika kuhusu umuhimu wa takwimu na kuongeza ufahamu kuhusu nafasi na mchango wa tasnia ya takwimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani aAfrika.
“Maadhimisho haya kwetu sisi watakwimu ni muhimu sana kwani tunayatuimia kuelimisha umma juu ya umuhimu wa takwimu katika mustakabali wa maendeleo ya taifa”amesema Chuwa.
