Akizungumza leo Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw. Valley Mutakyamirwa amesema kuwa dhamira yao ni kuendelea kujenga uwezo kwa wajasiriamali hao ili waweze kuchangika katika kutatua changamoto zinazowakabili kwa kuweka mikakati ya pamoja kati ya wanachama wa Taasisi hiyo.
“Wajasiriamali hawa ni wanachama wetu hivyo jukumu letu ni kuhakikisha kuwa tunashirikiana nao katika kuibua changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ambayo tunashirikiana na Serikali katika kuona namna bora yakuzitatua “; Alisisistiza Mutakyamirwa
Akifafanua amesema kuwa, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali ikiwemo kujenga miundombinu, kupunguza kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kutoka asilimia 20 hadi 18 hali inayoonesha dhamira ya dhati ya Serikali kuendelea kuimarisha mazingira ya wajasiriamali kufanya biashara.
Aliongeza kuwa Warsha hiyo inawasaidia wajasiriamali hao kufanya tathmini ya shughuli wanazofanya na kuja na mikakati ya pamoja itakayoasaidia katika kuimarisha Biashara hapa nchini.
Kwa upande wake Muwezeshaji kutoka Taasisi ya Best Dialogue Bi. Manka Kway akizungumzia kuanzishwa kwa Maktaba ya Mtandaoni itakayokuwa na taarifa zote kuhusu masuala ya wajasiriamali zikiwemo tafiti, machapisho,fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo, Utalii, Biashara, Uwekezaji, Viwanda na miundombinu.
Aliongeza kuwa kuwepo kwa maktaba hiyo kutasaidia kuimarisha na kusaidia kuinua kiwango cha Biashara hapa nchini kwa kuvutia wawekezaji na wajasiriamali wa ndani na nje ya nchi kuongeza uwekezaji na kuchochea maendeleo.
Pia aliwataka wajasiriamali kutumia fursa ya kuwepo kwa Maktaba hiyo kufuatilia taarifa mbalimbali zilizopo katika maktaba hiyo ya mtandaoni katika kutafuta fursa mbalimbali zinazoweza kuimarisha utendaji wa wajasiriamali hao na kukuza sekta husika.
Katika maktaba hiyo ya mtandaoni wawekezaji kutoka katika mataifa mbalimbali wanaweza kupata taarifa zitakazowawezesha kuja kuwekeza hapa nchini na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya Biashara na uwekezaji hapa nchini.
Warsha ya kuwajengea uwezo wajasiriamali ambao ni wanachama wa Taasisi ya Sekta Binafsi inafanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma ikilenga kuwajengea uwezo wajasiriamali hao ili kuongeza tija kwa wajasiriamali hao hapa nchini .
