Taasisi zagawiwa Sukari ya magendo


SERIKALI wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, imekamata sukari iliyoingizwa kwa njia ya magendo na kuigawa kwa taasisi mbalimbali.

Taasisi hizo ni shule za sekondari na msingi, Magereza, vituo vya kulelea watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Akizungumza wakati wa kuigawa sukari hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Zainabu Kawawa, alisema Wilaya ya Bagamoyo imejipanga kikamilifu kukomesha mianya yote ya kukwepa ushuru na kwamba kila anayejaribu kutumia bandari bubu sheria itamshughulikia.

Kawawa alisema serikali inahitaji kukusanya mapato kupitia vyanzo vyake, ili kuendesha masuala mbalimbali ya kimaendeleo katika jamii, hivyo anayekwepa kodi na ushuru ni mpinga maendeleo na serikali itamshughulikia.

Aliongeza kwa kuwataka wakuu wa shule kuitumia sukari hiyo kwa wanafunzi kama ilivyokusudiwa na si vinginevyo na kuonya kuwa atakayeitumia sukari hiyo kinyume cha kusudio, atachukuliwa haatua za kisheria.

Naye Ofisa Mfawidhi wa Kituo cha Forodha Bandari ya Bagamoyo, Raymond Mwanisawa, alisema wamemkabidhi Mkuu wa Wilaya sukari hiyo, ili agawe kwenye taasisi zenye uhitaji zikiwamo shule na vituo vya kulelea watoto.

Mwanisawa alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), bidhaa kama hizo zilizokwepa ushuru, Kamishna wa Forodha na Kodi ya Bidhaa nchini, anatoa kibali cha kugawa bidhaa hizo ili zisije kuharibika zilipohifadhiwa kwa muda mrefu.

Alisema sukari hiyo imekamatwa kufuatia doria iliyofanywa na maofisa wa forodha kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha bidhaa zote zinazoingizwa Bagamoyo zinalipiwa ushuru halali wa serikali.

Jumla mifuko 220 ya sukari ambayo kila mmoja ukiwa na kilo 50 amekabidhiwa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo ili kuzigawa kwa taasisi zenye uhitaji.

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items