KOCHA wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ Emmanuel Amunike, ameongeza dozi ya mazoezi ya timu hiyo iliyoweka kambi Afrika Kusini kujiandaa na mchezo wake wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) dhidi ya Lesotho huku akiingiza darasani kuwasoma wapinzani wao kupitia mikanda ya video.
Stars itaumana na Lesotho Jumapili ijayo kwenye mchezo ambao utatoa picha kamili ya safari ya Tanzania kufuzu kwenye fainali hizo zitakazofanyika Cameroon.
Akizungumza na Nipashe jana, Meneja wa Taifa Stars, Danny Msangi, alisema kocha Amunike kwa sasa anawafanyisha mazoezi mara mbili kwa siku na programu hiyo itaendelea mpaka Ijumaa watakapoanza safari ya kuelekea Lesotho.
“Maandalizi yetu yanaendelea vizuri, kwa sasa tunafanya mazoezi mara mbili kwa siku, asubuhi na jioni, lakini leo hii tumefanya uchambuzi wa mechi, tumeanza kuangalia mchezo wetu dhidi ya Lesotho na baadaye tumeangalia mikanda ya wapinzani wetu kuangalia mbinu zao na nini wachezaji wanatakiwa kukifanya,” alisema Msangi.
Alisema kocha amewaelekeza nini walikosea kwenye mchezo wa kwanza ambao walitoka sare ya bao 1-1 na kuwapa mbinu za kufanya kuwawezesha kupata ushindi.
Katika hatua nyingine, Msangi alisema wachezaji wa Stars wanaocheza nje ya Tanzania wameanza kuwasili kwenye kambi ya timu hiyo.
“Jana tumepokea wachezaji watatu ambao ni Abdi Banda, Rashid Mandawa na Hassan Kessy, leo (jana) tunatarajia kuwapokea Himid Mao kutoka Misri, Simon Msuva anayetokea Morocco pamoja na Shabaani Chilunda anayetokea Hispania,” alisema Msangi.
Stars inayoshika nafasi ya pili kwenye Kundi lao la L ikiwa na pointi tano nyuma ya kinara Uganda yenye pointi 10, inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kujisogeza karibu kabisa na nafasi ya kufuzu kwa fainali hizo za Afrika ambazo haijashiriki kwa miaka 34 sasa.
Endapo Stars itashinda mchezo huo na Uganda kuichapa Cape Verde Jumapili, kikosi hicho cha Amunike kitakuwa kumefuzu moja kwa moja kushiriki fainali hizo zitakazofanyika Cameroon mwakani kikishirikisha mataifa 24.
