.

12/06/2018

Waziri Ummy Mwalimu aagiza Afisa afya kuchunguzwa

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo wakati wa mkutano wa uhamasishaji kwa kujiunga na mfuko wa Bimba ya Afya
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Ummy Mwalimu amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Newala,  Aziza Mangosongo, kumchunguza Afisa Afya wa Wilaya hiyo maarufu kwa jina la Mama Flora kwa tuhuma ya rushwa aliyochukua kutoka kwa Bw.Shaib Mussa kama adhabu ya kutupa taka hovyo.

Hayo yamefuatia baada ya Mwananchi aliyejitambulisha kwa jina na Shaibu Musa kutoa malalamiko yake mbele ya Waziri ya kulipishwa shilingi elfu 50,000 na Bibi Afya huyo mwaka Jana.

Waziri Ummy alisema kuwa Watumishi wa Serikali hasa wa Sekta ya Afya ni lazima wajiepushe na vitendo vya Rushwa na kuacha tamaa zinazopelekea kuminywa kwa haki kwa baadhi Wananchi wanaotaka kupata huduma.

“Namtafuta mmoja ili nimtolee mfano kwa Tanzania nzima, bahati nzuri Mimi ni Mwanasheria, Kosa la jinai halina muda, hata kama ni 2017, tunataka huyu mtu afuatiliwe, achunguzwe kama kweli shilingi 50,000 iliingizwa kwenye Halmashauri au haijaingia, tunataka Mazingira masafi lakini ile hela iende Serikalini” alisema Waziri Ummy.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto yupo Mkoani Mtwara kwa ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya Pamoja na uhamasishaji kwa wananchi kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) na Leo hii yupo Wilayani ya Newala.