Na.Thabit Madai, Zanzibar.
Serikali ya Mkoa wa mjini Magharibi Unguja imesema imeridhishwa na ongezeko la kiwango cha ufaulu wa kidato cha nne kwa kipindi cha mwaka 2018 ikilinganishwa na mwaka 2017.
Imesema katika kipindi cha mwaka 2018 ongezeko hilo imefikia asilimia 70.43 ikilinganishwa na mwaka 2017 ambapo ilikuwa asilimia 55.88.
Akizungumza leo na waandishi wa habari ofisini kwake vuga, Mjini Unguja Mkuu wa Mkoa huo,Ayoub Mohammed Mahmoud alisema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 14.55 na kwamba hatua hiyo inatokana na juhudi zilizofanywa na uongozi wa serikali ya mkoa huo.
Mkuu huyo aliongeza kuwa katika ongezeko la ufaulu huo umefanikiwa kuziondoa skuli mbili za sekondari zilizokuwa katika shule 10 za mwisho zilizofanya vibaya na kwamba hatua hiyo ni matokeo chanya.
"Tumefanikiwa kuziondoa skuli mbili za sekondari ya Langoni na Mwenge ambazo mwaka 2017 zilikuwa katika skuli 10 za mwisho kitaifa hiyo ni moja ya mafainikio makubwa yaliyopatikana katika mwaka 2018" alieleza
Aidha alieleza kuwa mafaniko hayo yanatokana juhudi mbali mbali zilizofanywa na wadau wa sekta ya elimu pamoja na Serikali ya mapinduzi ya zanzibar katika kuondoa michango ya skuli ambapo ilikuwa na lengo la kupunguza ghsrama na kuongeza kiwango cha elimu zanzibar.
Hata hivyo Mkuu huyo alisema idadi ya wanafunzi waliopata ufaulu wa daraja la kwanza 147 na daraja la pili 638 na daraja la 3, 1341 na daraja la 4, 4317.
alisema katika kipindi hicho alifanikiwa kupunguza idadi ya wanafunzi waliopata ziro na wamefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaendelea na masomo ya kidato cha tano na sita zaidi ya elfu moja.
Aidha alisema serikali ndani ya mkoa wa Mjini Magharib utatoa zawadi ya Tablet ambazo zitakuwa na vitabu vya masomo kwa kidato cha Tano na sita kwa wanafunzi waliopata daraja la kwanza jumla yao 147.
Hata hivyo alisema kwa upande wa walimu walifaulisha wanafunzi hao watapewa zawadi ya kiasi cha milion 30 kwa ujumla wao.