Serikali imesema kuwa mwaka huu inatarajia kuajiri walimu wapya 6000 wa masomo ya Sayansi na Hesabu ambapo tayari kibali cha kuwaajiri walimu hao kimekwishatolewa.
Aidha Serikali inakusudia kuwapeleka walimu 11,000 wa masomo ya sanaa ambao ni wa ziada waliokuwa wakifundisha shule za sekondari kufundisha shule za msingi ili kukabiliana na upungufu wa walimu unaozikabili shule za msingi nchini.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu, Mwita Waitara ameyasema hayo katika Wilaya Chemba, mkoani Dodoma wakati akizungumza na watumishi kutoka Idara za Elimu ya Msingi na Sekondari kutoka Halmashauri hiyo.
Kauli hiyo ya Serikali inafuatia taarifa ya Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya wilaya ya Chemba bwana Josephat Ambilikile kumweleza Naibu Waziri kuwa Halmashauri ya Chemba ina upungufu wa walimu 808 kati ya walimu 1628 wanaotakiwa kufundisha katika shule za msingi 103 zilizopo katika wilaya hiyo.
Waitara alisisitiza kuwa Serikali kuanzia mwaka huu itakuwa ikiajiri walimu kila mwaka ili kufidia walimu wanaostaafu na pia kukabiliana na upungufu unaotokana na ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule za msingi kutokana na mwitikio wa wazazi kupeleka watoto wao shule kufuatia uamuzi wa serikali ya awamu ya tano kutoa elimu ya bila malipo.
“Tayari Mheshimiwa Rais Dkt John Pombe Magufuli amekubali walimu waajiriwe na kibali kimekwishatolewa hivyo walimu 6000 wa masomo ya sayansi na hesabu na pia walimu 11,000 ambao ni walimu wa ziada waliokuwa wakifundisha masomo ya sanaa katika shule za sekondari watapelekwa kufundisha shule za msingi,” alisema Mhe.Waitara.
