Dkt. Mary Mwanjelwa ataka huduma za TEHAMA zifike vijijini


Waziri wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa ametaka huduma za TEHAMA zifike kwa wananchi wa vijijini.

Dkt. Mwanjelwa ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha Pili cha Serikali Mtandao cha mwaka 2019 kilichofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma mkoani humo kwa viongozi waandamizi wa Serikali ikiwemo Makatibu Wakuu, wakuu wa Taasisi, mashirika na Idara mbali mbali za Serikali, wataalamu wa TEHAMA na watumishi wengine wa umma

"Tunaelewa wananchi wengi wanaishi vijijini, hivyo tuhakikishe huduma za TEHAMA na za serikali mtandao zinafika kwa wananchi kwa haraka na tuhakikishe tuna wataalamu wa kutosha wa TEHAMA na wa serikali mtandao,” amesema Dkt. Mwanjelwa.

Pia, ameongeza kuwa taasisi zote za umma zizingatie usalama mtandaoni katika hatua zote za kujenga na kutumia mifumo mbali mbali ya TEHAMA na zishirikiane na Wakala wa Serikali Mtandao katika kubuni na kutumia TEHAMA na matumizi ya serikali mtandao. Ameongeza kuwa utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao utakuwa ni kichocheo cha maendeleo ya TEHAMA nchini kwa kuwa itawezesha utoaji wa taarifa ufanyike kwa wakati na kwa haraka.

“Taasisi za umma zishirikiane na Wakala wa Serikali Mtandao kwenye hatua za awali za manunuzi ya vifaa, huduma na mifumo ya TEHAMA nchini ili taasisi husika iweze kupata huduma au vifaa stahiki kutoka kwa mzabuni husika badala ya kuita Wakala wa Serikali Mtandao wakati mambo yameharibika,” amesisitiza Dkt. Mwanjelwa.

Dk. Mwanjelwa amesema kuwa huduma za serikali mtandao zitumike kupunguza gharama za utoaji huduma ili kuboresha huduma za Serikali kwa wananchi wake ili kuweza kuendana na kauli mbiu ya kikao hicho isemayo, “Uwianishaji wa Rasilimali za TEHAMA kwa Maendeleo ya Viwanda,” kwa kuwa TEHAMA ni mtambuka na inatumika kwenye sekta nyingine za kiuchumi na kijamii.
Mpya zaidi Nzee zaidi