Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma ameomba wananchi wa mkoa wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kwenye Maonesho ya Wiki ya utoaji wa Elimu ya Sheria na kuiuliza maswali Mahakama hasa juu ya ucheleweshwaji wa kesi zao na kuahidi kuwa maswali hayo yatajibiwa ipasavyo.
Amebainisha hayo mara baada ya kutembelea maonesho hayo ambapo amewataka wananchi wenye malalamiko na maoni kuhusu utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania kujitokeza na kueleza changamoto ili ziweze kujibiwa.
“Nawakaribisha wananchi wenye nafasi kufika kwenye viwanja vya Nyerere Square ili waweze kuona Mahakama ya Tanzania inavyofanya kazi zake kwa kushirikiana na wadau, ni wakati mzuri wa kutathmini utendaji wa Mahakama katika kipindi cha mwaka moja yaani tangu 2018” alisema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu ameongeza kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja, Mahakama ya Tanzania imepiga hatua hasa kutokana na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika kesi. Wiki ya Sheria imeanza January 31 mwaka huu Jijini Dodoma na itamalizika February 5 ambapo siku ya Sheria nchini itaadhimishwa February 6 katika viwanja vya Chimala Jijini Dar es Salaam.
