Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Mahakama nchini kwa kufanya kazi kwa kasi na weledi katika kuhakikisha wananchi wanapata haki yao ambayo inahitajika.
Akizungumuza katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema kuwa katika miaka miwili iliyopita mahakama imepiga hatua na kufanya mabadiliko makubwa katika sekta Sheria nchini ikiwemo kutenda haki na kuongeza mapato kutoka Bilioni 1.62 mpaka bilioni 2.2.
“Natambua umuhimu wa Sheria katika ustawi na maendeleo ya Taifa letu, naipongeza sana Mahakama na Wadau wote wa Sheria nchini kwa mafanikio mliyoyapata, kuna mabadiliko mengi sana kwa sasa katika sekta sheria nchini”, Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema kuwa katika kutekeleza malengo ya usikilizaji mashauri Mahakama umeweza kusikiliza na kumaliza mashauri yalikuwa ya muda mrefu kwani mpaka sasa kuna mashauri 16 tu yenye muda wa miezi sita sawa na asilimia 0 katika mashauri 15,675 yaliyobakia Mahakama ya Mwanzo.
Katika kuimarisha sekta ya Sheria Rais Magufuli alisema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama ambapo hadi sasa imeweza kuteua Majaji 2 Mahakama ya Rufani, Jaji kiongozi na Majaji 12 wa Mahakama Kuu kwa mwaka 2018, huku mapema mwaka huu ikiteua Majaji 6 Mahakama ya Rufani na Majaji 15 Mahakama Kuu, idadi inayofanya kuwa na Majaji 73 wa Mahakama Kuu na Majaji 21 Mahakama ya Rufani.
Aidha Rais Magufuli alisema kuwa katika kuhakikisha mahakama inafanya kazi na kuongeza kasi zaidi Serikali imejikita pia katika kuimarisha miundombinu ya kufanyia kazi huku ikiwezesha ujenzi wa Mahakama 22 za Mwanzo, 20 Wilaya, 8 Mkoa na Mahakama Kuu 2 ambazo zitagharimu shilingi Bilioni 34.
Pia Rais Magufuli alizindua mahakama zinazotembea kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kuwafauta wananchi walioko mbali na Mahakama, likiwa na Televisheni ya kurekodi ushahidi, kamera, kipaza sauti, vifaa vya Tehama, printer na mashine ya kutolea photocopy, kabati na rifiti ya watu wenye mahitaji maalum, Mahakama hiyo ambayo kwa ujumla imegharimu milioni 470 itaanza kufanya kazi kwa mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam, lakini pia alizindua Mfumo wa Kuratibu mashauri ambao nao umegharimu milioni 191.
Naye Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma alisema kuwa siku zote Mahakama inapotoa haki inatekeleza suala la kulinda amani na kutekeleza ustawi wa jamii kwa ujumla.
