Jeshi la Polisi mkoani Pwani, limeweka bayana kuendelea kukaza uzi, katika kupambana na wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa kwa njia za magendo kwa lengo la kukwepa ushuru na kuisababishia Serikali kukosa mapato.
Kutokana na hatua hiyo Jeshi hilo limefanikiwa kukamata madumu 86 ya mafuta ya kula ambayo hayajalipiwa ushuru yakiwa yamehifadhiwa ndani ya stoo ya mfanyabiashara Mmas Athumani (35) mkazi wa Kongowe Kibaha mkoani hapo.
Kamanda wa polisi mkoani humo, (ACP) Wankyo Nyigesa amesema kuwa madumu hayo yamefikia jumla ya 107 yaliyokamatwa katika kipindi cha wiki moja.
“Taarifa tumezipata kutoka kwa raia wema, ambapo walieleza mafuta hayo yameingizwa nchini kupitia Bagamoyo na kukwepa ushuru wa serikali kisha kusafirishwa kwa njia za panya hadi kwenye stoo hiyo eneo la Kongowe “alifafanua Wankyo.
Alitaja mafuta ni dumu moja lita 20 aina ya jenau, madumu 26 ya lita 20 aina ya MTRA pamoja na madumu 59 ya lita 20 aina ya oki. Aidha Wankyo alisema, pia limekamata mifuko 18 ya sukari ambayo imeingizwa nchini kutoka nchi jirani kwa kukwepa ushuru.
