Waziri wa Madini, Doto Biteko leo, Februari 6, 2019 amekutana na watendaji na watumishi wa Tume ya Madini katika makao makuu ya Tume yaliyopo jijini Dodoma, lengo likiwa ni kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Tume.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Madini, Issa Nchasi na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula.
Wengine ni pamoja na Kamishna kutoka Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya, Wakurugenzi, Mameneja pamoja na watumishi wa Tume ya Madini.
Katika kikao hicho Waziri Biteko ametoa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na vituo vya ukaguzi wa madini ya ujenzi kufufuliwa, kikao cha kamati tendaji kukutana mara kwa mara kwa ajili ya kupitia na kuidhinisha maombi mbalimbali ya leseni za madini na watumishi kufanya kazi kwa uadilifu.


