Kocha wa timu ya taifa ya Uganda, Sébastien Desabre ameelezea maandalizi yao kuelekea mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Taifa Stars, saa 12 jioni utakaofanyika katika Uwanja wa taifa Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, Desabre amesema kuwa anajua kuwa wao wameshafuzu michuano ya AFCON na wanachotakiwa ni kuendeleza hatua hiyo.
"Maendeleo ya timu yetu katika hatua zinazofuata ni mazuri, tumekuwa ni miongoni mwa timu za kwanza kufuzu na kesho tutakuwa tunaendeleza maandalizi yetu ya hatua inayofuata ya AFCON", amesema kocha Desabre.
"Tanzania ina timu nzuri na kocha mzuri pia, tumeiona hata katika mchezo tuliocheza nao nyumbani. Najua kuwa wako katika 'pressure' kubwa ya kufuzu na kwa upande wetu tuna pressure ndogo lakini huu ni mchezo wa kimataifa, tutaonesha ushindani hata kama mchezo hautakuwa na faida sana kwetu", ameongeza.
