Na. Paschal Lucas, Mwanza
Mbunge wa jimbo la Magu mkoani Mwanza (CCM) Comredi Boniventula Kiswaga, amechangia jumla ya mifuko hamsini ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati inayojengwa na uongozi wa Gereza la Wilaya ya Magu.
Kiswaga ametoa mchango huo ikiwa ni kuunga mkono juhudi zilizoanzishwa na Uongozi wa Gereza Wilaya Magu katika kukabiliana na ukosefu wa zahanati katika makao makuu ya Wilaya hiyo.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Magu, Dr. Philemon Sengati alivutiwa na ubunifu wa uongozi wa Gereza katika kutatua changamoto za kijamii na kutoa msaada wa mbao mia moja zenye thamani ya zaidi ya milioni tatu na tayari ameshakabidhi kwa uongozi wa Gereza.
Hata hivyo kwa nyakati tofauti tofauti Mkuu wa Wilaya na Mbunge wameendelea kuihamasisha jamii ijitolee na kuunga mkono uanzishwaji wa ujenzi wa miundombinu mbalimbali wilayani humo ikiwemo zahanati, madarasa kama walivyojitolea waalimu wa shule ya sekondari Magu katika ujenzi wa darasa hususan katika makao makuu ya Wilaya ili kuendana na sera ya Serikali ya ujenzi wa zahanati kwa kila kijiji.
Ujenzi wa Zahanati hiyo ukikamilika inatarajiwa kuwahudumia wakazi wa eneo la mji mdogo wa Magu lenye kata tatu za Isandula, Itumbili na Magu mjini ambao hawana zahanati wala kituo cha afya, kwa takribani miaka 45 tangu Wilaya hiyo kuanzishwa.