Beki wa Yanga SC mwenye uwezo mkubwa Uwanjani Abdalah Shaibu, 'Ninja' ameeleza kuwa amekuwa akipambana na washambuliaji wengi bongo ila wanaompa taabu kuwakaba ni wawili ambao wanaitumikia timu ya Simba kwa sasa.
Beki huyo amesema kuwa amekuwa akiwadhibiti washambuliaji wengi bila matatizo ila anapokutana na miamba miwili amekuwa akitumia akili ya ziada pamoja na kipaji kuwazuia kwani hawatabiriki wakiwa ndani ya Uwanja.
"Meddie Kagere na John Bocco hawa ni washambuliaji ambao nikikutana nao uwanjani ninatumia akili nyingi na nguvu kuwazuia kwani hawatabiriki wakiwa uwanjani lolote linaweza kutokea.
"Bocco ana unafuu kidogo ninaweza kuhimili mikikimikiki yake ila huyo Kagere ni msumbufu na ana nguvu nyingi hali ambayo inahitaji umakini mkubwa kumkabili, ila licha ya ubora wao hainifanyi niwaogope kwani kazi yangu ni mpira na nikikutana nao ni lazima nijipange kuwazuia washambuliaji wote," amesema Ninja.
Yanga imecheza michezo 28 huku ikipoteza michezo mitatu pekee na kutoa sare michezo minne na imeshinda michezo 21 ipo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 67.
