Watu sita wamejeruhiwa baada ya roketi ya masafa marefu kurushwa katikati mwa Israeli. Roketi hiyo ilirushwa kutoka Ukanda wa Gaza.
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu anatazamiwa kufupisha ziara yake nchini Marekani ambayo alianza tangu siku ya Jumapili baada ya mazungumzo na Donald Trump.
"Kufuatia matukio ya usalama, nimeamua kufupisha ziara yangu nchini Marekani," Waziri Mkuu wa Israel amesema. Netanyahu, ambaye anatarajia kuwania muhula mwingine ifikapo Aprili 9, ameahidi kujibu kwa haraka mashambulizi hayo, ambayo ameyataja kama uhalifu usiokubalika.
Roketi hiyo ilianguka mapema asubuhi juu ya nyumba huko Mishmeret, kaskazini mwa Tel Aviv. Machi 14, roketi mbili zilrushwa katika mji wa Tel Aviv, lakini hazikusababisha uharibifu wala hasara yoyote, kwa mujibu wa mamlaka ya Israel, ambayo ilishtumu kundi la Hamas.
