Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kimepongezwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako kwa kuwa mfano kwa kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia vizuri mapato ya ndani katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Waziri Ndalichako ameyasema hayo wakati akizindua rasmi ukumbi mpya wa kisasa wa mihadhara katika Kampasi ya Kivukoni ambapo amesema Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kimeonyesha njia hivyo amezitaka taasisi nyingine za elimu kuiga mfano wa Chuo hiki kwa kuthamini mapato yake ya ndani na kuelekeza fedha hizo kwenye miradi ya maendeleo.
Waziri Ndalichako amekiagiza Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kujielekeza zaidi katika kutoa mafunzo ya uongozi na kuongeza kuwa kwa kushirikiana na Serikali wizara yake
itahakikisha kunakuwa na mfumo maalum wa kuhakikisha viongozi wanakuja kupata
mafunzo katika Chuo hiki.
Akisoma taarifa ya Chuo kuhusu mradi huo, Mkuu wa Chuo hicho Prof. Shadrack Mwakalila amesema Chuo kimeamua kujenga ukumbi wa kisasa wa mihadhara kwa kutumia vyanzo vya mapato ya ndani.
Prof. Mwakalila ameongeza kuwa ukumbi huo wenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 330 kwa
wakati mmoja pamoja na ofisi 8 za wafanyakazi hadi kukamilika kwake umegharimu kiasi cha Tsh. 1,150,666,161.78.
